Home » » ‘Walioua watu msikitini Mwanza watakamatwa’

‘Walioua watu msikitini Mwanza watakamatwa’

Written By Vuvuzela on Saturday, May 21, 2016 | 10:52:00 AMSERIKALI imeahidi kuwa vyombo vya dola, vitakamata wahalifu wote walioua watu watatu kwa mapanga msikitini huko Mwanza na kujeruhi wengine kadhaa.

Imeagiza jeshi la polisi kufanya msako usiku na mchana, kukamata wahalifu waliofanya mauaji hayo ya kinyama. Imesisitiza kwamba damu ya watu hao, waliouawa kikatili wakiswali msikitini wilayani Nyamagana haitapotea bure, kwani wahalifu wote watakamatwa.

Kauli hiyo ya Serikali ilitolewa bungeni mjini hapa juzi na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni. Masauni alisema serikali imesikitishwa na mauaji ya watu hao watatu, waliouawa msikitini katika wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza. Alisema mauaji hayo yameleta simanzi na majonzi makubwa kwa wakazi wa Mwanza na Watanzania kwa ujumla.

Masauni alisema kuwa Serikali inawapa pole wakazi wa Mwanza, viongozi wa mkoa na wilaya ya Nyamagana na mbunge wa jimbo hilo, Stanslaus Mabula.

Juzi kundi la watu wanaokadiriwa 15, walivamia Msikiti wa Masjid Rahman uliopo Ibanda Relini Mtaa wa Utemini Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana na kuua watu watatu kwa mapanga, ikiwemo imamu wa msikiti. Pia, walijeruhi waumini kadhaa waliokuwa wakiswali msikitini hapo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema watu hao walikuwa wamevalia mavazi ya kuficha uso wakiwa na mapanga, shoka na bendera nyeusi yenye maandishi meupe.

Waliouawa katika tukio hilo ni Imamu wa Msikiti huo, Feruz Elias (27) mkazi wa Ibanda Relini na Mbwana Rajabu (40), ambaye ni mfanyabiashara mkazi wa Ibanda. Mwingine ni Khamisi Mponda (40) ambaye ni dereva wa Kiwanda cha Samaki cha TFP mkazi wa Mkolani wilaya ya Nyamagana.

Kamanda Msangi alisema watu hao waliingia ghafla msikitini hapo wakati waumini wakiswali na kuamuru taa zizimwe; na waliwahoji waumini sababu za kuendelea kuswali, ilhali wenzao wamekamatwa na kushikiliwa na Polisi.

Kisha walianza kuwakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za miili yao, ambapo baadhi wamepata majeraha makubwa kichwani, shingoni na mikononi. Majeruhi ni Ismael Abeid (13) ambaye ni mwanafunzi wa Madrasa katika Shule ya Kiislamu ya Jabar Hila iliyoko Nyasaka Manispaa ya Ilemela. Anatibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana.

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts