Home » » Binti aliyemwandikia barua Rais Obama azuru bungeni

Binti aliyemwandikia barua Rais Obama azuru bungeni

Written By Vuvuzela on Sunday, June 5, 2016 | 11:52:00 AM


MWANAFUNZI wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Mlowa wilayani Iringa, Eva Tolage (16) ambaye mwaka jana alimwandika barua Rais Barack Obama wa Marekani akielezea kero zinazowakabili watoto wa kike katika kijiji chake, juzi alitembelea bungeni mjini hapa, huku akiwasisitiza viongozi wa kisiasa kuwajibika kwa kutekeleza ahadi zao ili kuondoa kero zinazowakabili wananchi.

Eva aliyepata pia fursa ya kukutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi mbalimbali alisema jambo hilo hakulitarajia, kwani wakati anaandika barua hiyo hakufahamu kuwa itamfikia Rais Obama na kujibu.

Alisema viongozi wa kisiasa wana wajibu mkubwa wa kusimamia ahadi zao ili kuondoa kero vijijini hasa upatikanaji wa maji. Akizungumza wakati wa mahojiano na waandishi wa habari, alisema kero ya maji ni kubwa kijijini kwao ambapo watu na mifugo wamekuwa wakichangia maji.

“Maji ni adimu shuleni, yanapopatikana hadi kijijini kwetu ni kilometa saba hali inayofanya wasichana waishi katika mazingira hatarishi zaidi. Unaweza kupata vishawishi vya wavulana njiani na ukajikuta umepata ujauzito na kushindwa kuendelea na shule.

“Niliamua kumuandikia barua Rais Obama ili atusaidie kupata maji, nilipoandika barua hiyo nikawapatia Shirika la Health Development, lakini nilipopata taarifa kuwa barua hiyo imemfikia Rais Obama nilisikia furaha kwani ni jambo la ajabu sikulitegemea,” alisema.

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mlowa, anakosoma Eva, Denis Myovela alisema wamefurahishwa na ujasiri wa mtoto huyo na wanategemea shule yao itapata maji.

Meneja wa kampeni ya Simama na Eva, Oscar Kimario alisema barua iliyoandikwa na Eva ilisomwa kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa na Rais Obama akihimiza viongozi kutekeleza majukumu yao.

Eva aliandika barua baada ya kumaliza elimu ya msingi akiwa na miaka 15 wakati wa ukimalizika utekelezaji wa Mpango wa Malengo ya Milenia (MDGS) na Rais huyo akaijibu katika mkutano wa 70 wa Baraza la Umoja wa Mataifa wa Septemba, mwaka jana uliojadili Maendeleo Endelevu ya Dunia.

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts