Get the latest updates from us for free

Home » » Mfungo waanza, bei za bidhaa zapanda

Mfungo waanza, bei za bidhaa zapanda

Written By Vuvuzela on Wednesday, June 8, 2016 | 6:40:00 AM
WAKATI leo Waislamu kote nchini wanaanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, wafanyabiashara katika baadhi ya masoko jijini Dar es Salaam wamesema kuwa bidhaa zinazotumiwa kwenye mwezi huo baadhi zimepanda bei

Katika Soko la Kariakoo, bidhaa za ndizi, viazi na magimbi zimepanda huku kwenye masoko ya Ilala na Buguruni bidhaa hizo bei zake zikiwa hazijapanda kwa kile kilichoelezwa kuwa bidhaa nyingi ndio msimu wake.

Mfanyabiashara wa Soko la Kariakoo, Ashura Juma alisema bei hizo zimepanda kwani mkungu mmoja wa ndizi kwa sasa unauzwa kuanzia Sh 20,000 hadi 50,000 wakati awali walikuwa wananunua Sh 20,000 hadi 40,000.

Juma alisema kutokana na kupanda kwa bei hizo, wanalazimika na wao kupandisha bei na kwamba ndizi tatu wanauza kwa Sh 1,000. Pia alisema mazao ya magimbi hununua kwa gunia Sh 80,000 wakati awali walikuwa wananunua kwa Sh 50,000.

Mfanyabiashara katika Soko la Ilala Boma, Mussa Hassan alisema bei za vyakula hazijapanda kwa kuwa bidhaa nyingi ndio msimu wake. Alisema bei hizo zinaweza kupanda kuanzia leo na siku zinazofuata kwani ndio siku ambayo mfungo unaanza.

“Mimi nauza mchele, bei ni Sh 2,000 hadi 2,200 ndio bei ambayo imezoeleka hivyo huwezi kusema kwamba imepanda kwani sitegemei kupandisha bei zaidi tunaweza kupunguza bei kwa kuwa ndio msimu wa mavuno,” alisema Hassan.

Pia alisema kupanda kwa bei inategemea na msimu kwani kuna wakati bidhaa zinakuwa zinapatikana kwa shida na mwezi wa Ramadhani unaanza hivyo wanavyopandisha bei, watu wanasema wamepandisha sababu ya mfungo.

Mfanyabiashara wa viazi sokoni hapo, Zainabu Suleiman alisisitiza kuwa bei hizo hazijapanda kwa kuwa bado wanauza fungu moja Sh 1,000 na Sh 2,000. Alisema mazao mengi ya vyakula ndio msimu wake na kusisitiza kuwa wakiongeza bei hizo watapata dhambi kwa kuwa watu wanaofunga hawapaswi kuteseka na bei.

“Njoo Jumatano au Alhamisi labda bidhaa hizi zinaweza kupanda bei lakini hadi leo bado hazijapanda. Mfano magimbi, hapa tunauza kwa fungu Sh 1,000 hadi Sh 2,000 ni bei ya kawaida kwa kipindi chote hiki,” alieleza Zainabu.

Aidha, katika soko la Buguruni, bei za bidhaa hizo hazijapanda huku mazao mbalimbali ikiwemo muhogo kutoka mashambani ikishushwa kwa wingi na bei yake ni Sh 1,000 hadi 2,000 kwa fungu. Wafanyabiashara wa masoko hayo wamesema kuwa bidhaa hizo zitaendelea kufurika kwenye soko hilo kuanzia leo.

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts