Home » » Serikali Kuanza Msako Mkali wa Dawa na Vipodozi Feki

Serikali Kuanza Msako Mkali wa Dawa na Vipodozi Feki

Written By Vuvuzela on Thursday, June 30, 2016 | 6:39:00 PM

 
Serikali kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imesema hivi karibuni itaanza msako mkali wa kuwatafuta na kuwakamata wauzaji wa dawa zinazokatazwa pamoja na vipodozi vikali ambao wanajitangaza kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.

Hayo yamesemwa na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Umma kutoka TFDA Bi. Gaudensia Simwanza wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hii kuhusu kuibuka kwa watu wanaotangaza  biashara ya dawa na vipodozi ambavyo Serikali imevipiga marufuku. 


Akitaja bidhaa hizo Bi. Simwanza alisema ni pamoja na dawa za kuongeza ukubwa wa viungo vya mwili, kupunguza uzito wa mwili na vipodozi vyenye kemikali za kuchubua ngozi bidhaa ambazo zinasababisha madhara makubwa kwa binadamu ikiwemo ugonjwa wa Saratani.

“Kumezuka wafanyabiashara holela wanaotumia mitandao ya kijamii kama vile Instagram, Facebook, Whatsup Groups na kwengineko  kutangaza biashara ya dawa na vipodozi vyenye kemikali hatari ambavyo vimepigwa marufuku na TFDA hivyo wanaohusika wajiandae, hivi karibuni tutaanza kuwashughulikia.” Alisema Simwanza. 

Alibainisha kuwa bidhaa hizo nyingi hazijathibitishwa na kupewa kibali na TFDA hivyo wauzaji wanakiuka Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura ya 219 inayowataka wafanyabiashara wote wa bidhaa hizo kuzisajili kabla hazijaenda kwa  mtumiaji na kutofanya hivyo ni kwenda kinyume na Sheria.

Alieleza kuwa TFDA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wameandaa mkakati madhubuti wa kuhakikisha wanawabaini na kuwakamata wafanyabiashara wote wanaouza dawa na vipodozi hivyo kupitia mitandao na kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafikisha mahakamani au kuwatoza faini. 

Wengi wa wafanyabiashara hao hawaweki anuani za maeneo wanayopatikana na hawana maduka rasmi bali huweka namba za simu za mkononi lakini kwa kutumia vyombo vya dola tutawabaini tu na kuwatia mbaroni.” Alisisitiza Simwanza.

Kwa upande wake Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Innocent Mungy amewatahadharisha watumiaji wa huduma za mawasiliano hasa matangazo ya biashara kuwa makini na matangazo hayo kwani baadhi ya wafanyabiashara hizo wanaweza kuwa ni watu wenye nia mbaya. 

Hivi karibuni kumeibuka wimbi la wafanyabiashara wa dawa mbalimbali pamoja na vipodozi ambao wanajitangaza kupitia mitandao ya kijamii na kuna baadhi ya watu wananunua bidhaa hizo bila ya kuhakikisha usalama wake jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts