Home » » Basata Wafungia Wimbo Wa ‘Pale Kati Patamu’ Wa Ney Wa Mitego.

Basata Wafungia Wimbo Wa ‘Pale Kati Patamu’ Wa Ney Wa Mitego.

Written By Bigie on Saturday, July 16, 2016 | 2:53:00 PM


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeufungia rasmi wimbo wa ‘pale kati patamu’ ulioimbwa na Msanii Ney wa Mitengo kutokana na ukiukwaji mkubwa wa maadili.
 
Msanii huyu amekuwa na tabia na mienendo yenye kuchafua Sekta ya Sanaa yeye binafsi kupitia kutoa kazi chafu na kufanya maonesho yenye kukiuka maadili. Kazi zake zikikiuka maadili na kudhalilisha utu wa mwanamke sambamba na kutoa lugha za matusi na za kudhalilisha watu wa kada mbalimbali.

Ieleweke kwamba kwa mujibu wa kifungu namba 4(L) cha Sheria ya BASATA namba 23 ya mwaka 1984, Baraza limepewa jukumu la kuhakikisha linalinda maadili miongoni mwa wasanii wanapokuwa jukwaani au wanapobuni kazi yoyote ya sanaa.

ikumbukwe kwamba BASATA limeshamuita na kumuonya msanii huyu mara kadhaa kutokana na tabia yake ya kutoa kazi zisizokuwa na maadili na aliahidi kubadilika na kuachana na tabia hiyo.

Kwa hiyo kuendelea kwake kufanya matukio haya kwa makusudi ni uthibitisho kwamba hajabadilika na kwa maana hiyo ameendelea kuidhalilisha Sanaa na wasanii wa kitanzania wenye kujitambua na kuiheshimu kazi ya sanaa kama kazi nyingine. 

Kwa sasa Msanii huyu ametoa wimbo mwingine wa Pale Kati patamu ambao uko mitandaoni ukipambwa na picha chafu zinazoonesha mwanamke akiwa mtupu yaani uchi wa mnyama.

Kwa mantiki hii BASATA halitavumilia wasanii wachache ambao wanataka kuigeuza tasnia ya sanaa na wasanii genge la wahuni wasio na staha na wanaojipanga kuibomoa jamii. BASATA linapenda kueleza ya kufuatayo
 
• BASATA linatamka kuwa limeufungia wimbo huu rasmi kutumika kwa namna yoyote ile.
• Aidha pamoja na adhabu ya kufungia wimbo huu hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
 
Aidha, BASATA linawataka Wasanii wote nchini kufuata sheria, kanuni na taratibu mara wanapotengeneza kazi zao.
SANAA NI KAZI, TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI

Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI.

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts