Home » » John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi kwa Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai

John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi kwa Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai

Written By Vuvuzela on Monday, July 4, 2016 | 12:20:00 PM


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai kufuatia kifo cha Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Kilindi Mkoani Tanga Mhe. Beatrice Shelukindo kilichotokea jana tarehe 02 Julai, 2016.

Mhe. Beatrice Shelukindo ambaye amewahi kuwa Mbunge Bunge la Afrika Mashariki na baadaye kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vipindi viwili mfurulizo hadi alipostaafu mwaka jana 2015, amefariki dunia akiwa nyumbani kwao Njiro Mkoani Arusha.

Katika salamu zake Rais Magufuli amesema taifa limempoteza mtu aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo hususani alipokuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwawakilisha wananchi wa Jimbo la Kilindi na Mkoa wa Tanga.

“Mhe. Beatrice Shelukindo alikuwa kiongozi shupavu, ambaye siku zote alisimama kidete kupigania maendeleo ya wananchi na kutetea rasimali za taifa.

“Kupitia kwako Mhe. Spika Job Ndugai naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wote wa marehemu na pia kwa wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” Amesema Rais Magufuli.

Dkt. John Pombe Magufuli pia amewaombea wote walioguswa na kifo cha Mhe. Beatrice Shelukindo kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki cha kuondokewa na mpendwa wao na amemuombea marehemu apumzishwe mahali pema peponi, amina.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
03 Julai, 2016

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts