Home » » Kangi Lugola Aionya Jamhuri Kumsotesha Mahakamani

Kangi Lugola Aionya Jamhuri Kumsotesha Mahakamani

Written By Vuvuzela on Tuesday, July 5, 2016 | 1:01:00 PM


MBUNGE wa Mwibara, Kangi Lugola, anayekabiliwa na mashtaka ya kuomba rushwa ya Sh milioni 30, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itoe onyo kwa kitendo cha upande wa Jamhuri kuahirisha kesi mara kwa mara.


Licha ya Lugola, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Mvomero, Ahmad Saddiq (53) na wa Lupa, Victor Mwambalaswa (63).

Lugola alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba, baada ya Wakili wa Serikali, Dennis Lekayo kuahirisha kesi hiyo kwa kuwa waendesha mashitaka katika kesi hiyo hawapo.

Awali, Wakili Lekayo alidai, kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali lakini aliomba ipangiwe tarehe nyingine kwa kuwa mawakili hawapo.

Lugola aliomba Mahakama ikemee tabia hiyo kwa kuwa ofisi ya waendesha mashitaka ina watu wengi hivyo ingeweza kutoa wengine kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali. Aliendelea kudai kuwa, kitendo cha kuahirisha kesi hiyo mara kwa mara, kinawanyima haki yao ya msingi ya kufanya shughuli za kibunge.

“Kwa kuwa imekuwa kawaida washtakiwa wanapokuwa watoro, Mahakama inawaita ili wathibitishe, kwa nini hawajafika na wakati mwingine wanachukuliwa hatua hivyo naomba mahakama itoe onyo kwa upande wa Jamhuri,” alidai Lugola.

Baada ya maelezo hayo Wakili Lekayo aliiomba Mahakama iwawie radhi na kuahidi watafanya haraka kesi iendelee. Hakimu Simba alisema hoja ya mshtakiwa ni ya msingi kwani kama mwendesha mashitaka aliondoka, alitakiwa alete wengine. Aliwataka wasirudie kufanya hivyo.

Kesi imeahirishwa hadi Julai 12 mwaka huu kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Wabunge hao wanadaiwa wakiwa wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, waliomba na kushawishi kupewa rushwa ya Sh milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Gairo, Mbwana Magotta kama kishawishi cha kutoa mapendekezo ya hati safi kwa halmashauri hiyo.

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts