Home » » Maghembe: Tanzania Haitegemei Kenya Kupanga Kodi Zake

Maghembe: Tanzania Haitegemei Kenya Kupanga Kodi Zake

Written By Vuvuzela on Monday, July 4, 2016 | 9:18:00 AM


Wakati Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amesema Tanzania haitegemei Kenya kupanga kodi kwa maendeleo ya wananchi, amebainisha kuwa Serikali inafuatilia taarifa kuwa baadhi ya mawakala wa utalii nchini, wanafungua akaunti nchini humo kukwepa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). 

Profesa Maghembe alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki kufuatia malalamiko ya mawakala wa Utalii wanaodai hatua ya Serikali kutoza VAT kwenye utalii kutaathiri sekta hiyo.

Mawakala hao wamekaririwa na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, wakidai watalii wengi wamesitisha safari zao na wengi wameamua kwenda Kenya kwa vile nchi hiyo imeondoa VAT.

Taarifa hizo zilidai hatua hiyo ya Serikali imesababisha watalii 8,000 kusitisha safari zao na kufanya Tanzania kupoteza mapato ya Sh13 bilioni. 
Mtendaji Mkuu wa chama cha mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), Cyril Arko alisema wanachama wao walishapokea maombi ya safari (bookings) mwaka mzima nyuma na wengine kulipwa kabisa, hivyo ni vigumu kurudi kumwambia mteja kuwa kuna mabadiliko, ndio sababu wakaenda Kenya. 

Arko alisema watalii wameamua kwenda Kenya kwa sababu nyumbu ni wale wale wanaotoka Serengeti na kuingia Masai Mara, Kenya, lakini faida ya Kenya ni kwamba hakuna kodi ya VAT. 

Kauli ya Profesa Maghembe Akijibu malalamiko hayo, Waziri Maghembe alisema Tanzania si koloni la Kenya, kwamba kila mipango yake ya maendeleo itegemee taifa hilo. 

“Kenya siyo sehemu ya Tanzania na sisi (Tanzania) si koloni la Kenya. Kenya ni nchi tofauti, Uganda ni nchi tofauti, Uingereza  ni nchi tofauti,” alisema Profesa Maghembe na kuongeza;“Hizi ni kodi ndani ya Tanzania. Kenya ina mazingira tofauti kabisa na Tanzania. Hatuwezi kupanga kodi kwa maendeleo ya nchi yetu tukiwatazama wao,” alisema. 

Kwa mujibu wa Profesa Maghembe, katika kipindi cha miaka minne mfululizo, idadi ya watalii wanaotembelea Kenya imeendelea kupungua kutoka milioni mbili hadi milioni 1.3 mwaka jana.

“Na katika kipindi hicho huku kwetu wamekuwa wakiongezeka kutoka 800,000 hadi 1.2 milioni,” alisema. 

“Kule (Kenya) wana sababu  ya kuondoa VAT ili waone kama watavutia watalii wasiendelee kupungua. Hapa tulikuwa hatuna kodi hata siku moja. Hili jambo linapotoshwa sana,” alisisitiza. 

Profesa Maghembe alisema kinachoonekana ni kama kuna propaganda na mgomo baridi kutoka kwa baadhi ya mawakala wanaotaka kuihadaa dunia ili ione Tanzania kutoza VAT ni tatizo. 

Hata hivyo alisema Serikali inafuatilia kuangalia mwenendo kwa mwezi mmoja, miezi miwili ili kuona hali inakwendaje na baada ya kufanya tathmini ya kina, Serikali itatoa taarifa kwa umma. 

Alitolea mfano kuwa kuingia hifadhi ya Arusha ni Dola 45 za Marekani na Serikali ikitoza asilimia 18 ya VAT, ada ya kuingia katika hifadhi hiyo kwa siku inakuwa Dola 53.10, ambayo bado ni ndogo. 

“Sasa kusema kati ya Dola 45 na Dola 53 basi itafanya mtalii kutoka Marekani asije Tanzania hii ni dhana ngumu kuelewa. Serikali itafuatilia jambo hilo kwa kina,” alisema Waziri.

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts