Home » » Paul Makonda atoa wiki mbili kwa Wakuu wote wa Wilaya katika mkoani Dar

Paul Makonda atoa wiki mbili kwa Wakuu wote wa Wilaya katika mkoani Dar

Written By Vuvuzela on Tuesday, July 5, 2016 | 8:02:00 AM


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa wiki mbili kwa wakuu wote wa wilaya mkoani kwake, kuhakikisha wanatengeneza mpango kazi, utakaowezesha kuwatumikia wananchi.

Makonda alitoa agizo hilo jana wakati akiwaapisha wakuu hao, walioteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli kushika wadhifa huo. Alisema kutengenezwa na kukamilika kwa mpango kazi huo katika kila wilaya, kutawasaidia kutengeneza pia wa mkoa.

“Someni vizuri ilani ya Chama Cha Mapinduzi na ahadi zote za mwaka 2015/2020, pitieni hotuba ya Rais ambayo iliainisha vipaumbele vyote. Someni mazingira ya kazi katika maeneo yote mliyopewa kwenda kuwatumikia wananchi mkifanya hivyo tunaamini tutaweza kuja kutengeneza mpango kazi wa mkoa,” alisema Makonda.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kila baada ya siku 90 wakuu hao wa wilaya, watakuwa wakijieleza kwa wananchi kuhusu kazi walizopewa katika maeneo yao na kwamba atakayeshindwa, atafutiwe wilaya nyingine.

Alisema shughuli hiyo, itakuwa ikifanyika kwenye ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. Wakati huo huo ametoa wiki moja kwa wakuu hao wa wilaya, kuhakikisha maeneo yote ambayo yalikuwa yakifanya biashara za shisha, yamefungwa.

Shisha imekuwa tatizo hapa nchini. Nataka mlifanyie kazi kwa uzito zaidi suala hili kila mtu ahakikishe hakuna biashara ya shisha katika wilaya yake,” alisisitiza Makonda.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kuapishwa , wakuu hao wa wilaya, wamesema watahakikisha wanafanya kazi zao za kuwatumikia wananchi kwa weledi.

Walimuahidi mkuu wa mkoa kutimiza yote aliyowaagiza wafanikishe kutengeneza Dar es Salaam mpya. Akizungumzia vipaumbele atakavyosimamia wilayani kwake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alitaja ujenzi wa barabara zenye ubora na udhibiti wa ombaomba.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgadilwa alisema kipaumbele kikubwa atakachoanza nacho ni kushughulikia ugawaji wa wilaya hiyo, ikiwemo kubaki kwa madiwani na vyanzo vya mapato na kuitangaza wilaya hiyo ili wananchi waitambue.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felex Lyaviva alisema ili kukabiliana na rushwa ambayo ni changamoto nchini , ataanzisha vikundi mbalimbali ikiwemo vikundi vya akinamama na vijana wananchi wawe na shughuli ya kufanya kuondoa mianya ya rushwa.

“Rushwa ni tamaa wapo wafanyakazi wanaoona ni sehemu ya maisha yao bila kuomba rushwa hawawezi kufanya kazi. Nitatoa namba yangu kwa mwananchi yeyote atakayeombwa rushwa awasiliane na mimi, lazima vitendo hivi tuviondoe,” alisema

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts