Home » » Utoaji risiti wazua utata Sabasaba

Utoaji risiti wazua utata Sabasaba

Written By Vuvuzela on Tuesday, July 5, 2016 | 8:42:00 AM


SUALA la utoaji risiti kwa bidhaa zinazonunuliwa katika Maonesho ya 40 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere katika Barabara ya Kilwa, limezua utata baada ya wajasiriamali wanaoshiriki maonesho hayo kurudishiwa bidhaa zao kutokana na kutokuwa na risiti.

Katika lango la kuingilia uwanjani hapo ni lazima ufanyiwe uchunguzi maalumu kwa ajili ya usalama. Lakini unapotoka lazima pia ufanyiwe uchunguzi wa bidhaa ulizonunua, kuhakikisha umepatiwa risiti za mfumo wa kielektroniki (EFDs) au risiti ya kawaida lakini yenye TIN namba.

Kutokana na hatua hiyo, ni jambo la kawaida kuwaona wananchi wenye bidhaa hizo, wakiziacha lango la kutokea na kukimbilia katika maduka waliyonunua kudai risiti na kama maduka hayo hayana risiti, wanalazimika kurudisha bidhaa. Matangazo yanayotolewa na Tantrade katika maonesho hayo, yanaeleza kuwa bidhaa yoyote inayonunuliwa katika maonesho hayo, lazima iwe na risiti yenye TIN namba.

Wengi wa waathirika hao ni wajasiriamali kutoka mikoani waliofika na bidhaa zao, lakini sasa hata mchaichai uliofungwa na kuuza Sh 500 wanatakiwa kutoa risiti na ambao hawana wanarudishiwa.

Wakizungumza nasi, Mkurugenzi wa Moringa Natural Product kutoka Arusha, Christina Msapala alisema wamekumbana na changamoto hiyo kwa kurudishiwa picha anazouza kutokana na kutokuwa na risiti. Msapala alisema kwa siku mbili alipata wateja wa Sh 40,000 kila mmoja waliyonunua picha tatu za kiasili lakini walirudishwa wote.

Alisema aliacha risiti zake ili kusubiria mashine za EFDs zinazotolewa bure kufika mikoani, lakini kufika hapo aliambiwa zinahitajika hivyo kumlazimu kutuma wenzake wamuagizie risiti zenye TIN namba. “Ingekuwa vyema wangetufafanulia mapema tangu tulipokuwa tunajiorodhesha kushiriki lakini sasa imekuwa changamoto kubwa,’’ alisema.

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts