Home » » Mabasi ya mikoani kugoma Jumapili

Mabasi ya mikoani kugoma Jumapili

Written By Bigie on Wednesday, August 17, 2016 | 12:31:00 PM


CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kimesema kitasitisha huduma ya kusafirisha abiria kwenda mikoa yote nchini Jumapili ili kufanya ukaguzi wa mabasi yake, hatua ambayo itakuwa sawa na mgomo.

Aidha, Taboa imesema inapinga uamuzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kutangaza kuyafungia mabasi yote ya kampuni ya City Boy badala ya moja ambalo lilisababisha ajali mkoani Singida hivi karibuni.

Julai 4, mabasi mawili ya kampuni hiyo yaligongana uso kwa uso na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 30 wilayani Manyoni mkoani Singida.

Taboa imesema pia itaipeleka serikali mahakamani kutokana na kufungiwa kwa mabasi hayo kwani kwa mujibu wa sheria, aliyetakiwa kulifungia ni waziri mwenye dhamana na si Sumatra kama ilivyofanyika.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kumaliza kikao cha dharura cha wamiliki wa mabasi ya mikoani, Katibu wa Taboa, Enea Mrutu, alisema hawatakatisha tiketi kuanzia Jumapili ili kujipa muda wa kukagua mabasi yao kama yana uwezo wa kufanya safari ama la.

"Tumeamua kwa pamoja kuwa, kwa sababu tayari tumeshafanya 'booking' ya abiria, kuanzia Agosti 21 mwaka huu, tuanze kufanya ukaguzi wa mabasi yetu kote nchini ili yale ambayo hayana sifa yakae pembeni na yale yanayostahili kusafirisha abiria yafanye hivyo, kuliko utaratibu huu wa serikali wa kuyafungia yote bila kujali gari lililohusika kwenye ajali," alisema Mrutu.

Aidha alisema wanapinga vikali agizo la Sumatra la kuyafungia mabasi 60 ya kampuni 12 kwa makosa ya kusababisha ajali na wanataka mabasi yanayohusika pekee ndio yafungiwe.

Alizitaja kampuni zilizofungiwa mabasi yake kuwa ni Mohamed Trans, City Boy, Ota High Class, Kisbo Safari, Kisbo Express, Lubonelo na Kanda Safari.

Mrutu pia alisema kikao kicho kilipinga azimio la serikali kutaka mabasi yanayoenda masafa marefu kama mikoa ya Mwanza na Mbeya kutumia siku mbili na badala yake yatumie siku moja kama ilivyokuwa awali.

Alitaja azimio la tatu kuwa ni kufunga mfumo maalum wa udhibiti wa magari (Car Track System) ambao utaunganishwa na ule wa Sumatra ili kuliona gari lilipo kwa lengo la kudhibiti ajali.

Aidha, Mrutu alisema wamekubaliana mabasi yote yatatembea kilometa 80 kwa saa moja na 50 pale inapohitajika kama kwenye matuta ili kuepuka ajali.

Alisema wamekubaliana pia dereva atakayehusika kutembea zaidi ya mwendo waliokubaliana, afukuzwe kazi na kumchukulia hatua stahiki.

"Kama magari yetu tutayafanyia ukaguzi na pia kufunga kifaa cha kulionyesha basi na kupunguza mwendo, hakuna haja tena ya kutaka tusafiri zaidi ya siku moja... maeneo wanayoona kuna hatari ya usalama ni bora yakasubiriana na askari wakayasindikiza mpaka yanapokwenda," alisema.

Aliendelea kueleza kuwa wamekubaliana Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, awahakikishie hakuna askari atakayedai mabasi hayo rushwa.

Mrutu alisema wamekubaliana mabasi yasikaguliwe kila kituo ili kuepuka kupoteza muda wakati wakisafiri kwenda mikoani ambako kunasababisha madereva kutembea mwendo kasi ili kuokoa muda waliopoteza njiani.


Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts