Home » » UVCCM waanza kutumbuana, baadhi wasimamishwa wengine wafukuzwa kazi.

UVCCM waanza kutumbuana, baadhi wasimamishwa wengine wafukuzwa kazi.

Written By Vuvuzela on Monday, August 15, 2016 | 11:38:00 AM

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umewasimamisha kazi na kuwafukuza viongozi wake wa Mkoa wa Iringa huku aliyekuwa Katibu Mkuu wa umoja huo, Sixtus Mapunda, akipelekwa mbele ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ili aweze kujadiliwa.

Mapunda ambaye pia ni Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), anatuhumiwa kukwapua hati za  viwanja vya UVCCM bila idhini za vikao husika.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema viongozi hao wamesimamishwa na wengine kufukuzwa kazi kutokana na tuhuma za kuuza shamba linalomilikiwa na umoja huo lililopo eneo la Igumbilo mkoani Iringa.

Alisema ripoti ya uchunguzi inaonesha kuwa shamba la UVCCM namba 454  lenye ekari 2,10 l limeuzwa kwa mtu aliyetambulika kwa jina la Suhail Ismail kinyume cha sheria na utaratibu wa chama.

Alisema Baraza Kuu la UVCCM Taifa linamsimamisha Seki Kasuga,  ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM na Mjumbe wa Baraza Kuu  kutoka Mkoa wa Iringa.

Mbali na vigogo hao mwingine aliyekumbana na tumbuatumbua hiyo ni Mkuu wa Idara ya Uchumi, Uwezeshaji na Fedha, Omar Suleiman ambaye pia ni Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Mjini- Zanzibar.

“Pia yupo Ally Nyawenga ambaye alikuwa Kaimu Katibu Mkuu UVCCM Mkoa wa Iringa. Huyu amefukuzwa kazi kwa kuuza viwanja vya UVCCM kisha kuzigawa fedha alizozikusanya kwa baadhi ya viongozi wa CCM.

“Baraza Kuu la UVCCM Taifa limeiagiza sekretarieti ya UVCCM kumwandikia barua ya kumfukuza kazi Upendo Kinyunyu ambaye ni Katibu Muhtasi ambaye kwa makusudi aliamua kupotosha taarifa zote alizotoa kwa kamati ya uchunguzi ili kamati ishindwe kubaini ukweli,” alisema Shaka.

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts