Home » » Rais Magufuli na mkewe Mama Janet wakabidhi msaada wa Sh mil 5 ya matibabu ya Mtoto anayeotwa na nyama kichwani

Rais Magufuli na mkewe Mama Janet wakabidhi msaada wa Sh mil 5 ya matibabu ya Mtoto anayeotwa na nyama kichwani

Written By Bigie on Tuesday, December 6, 2016 | 7:28:00 AM


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli jana  tarehe 5 Desemba, 2016 wamekabidhi msaada wa Shilingi Milioni 5 kwa ajili ya kusaidia matibabu ya mtoto Haidari Bonge mwenye umri wa miaka 9 anayesumbuliwa na tatizo la kuota nyama kichwani, kinywani na machoni.

Fedha hizo zimekabidhiwa kwa Mama wa mtoto huyo Sauda Kassim  na Kaimu Mnikulu Ndugu Ngusa Samike kwa  niaba ya Rais Dokta Magufuli katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo mtoto huyo anapatiwa matibabu.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi fedha hizo, Kaimu Mnikulu Ndugu Ngusa  Samike alisema Rais Dkt. Magufuli ameguswa baada ya kutazama kipengele cha Hadubini “Habari kwa Kina” kilichorushwa hewani katika taarifa ya habari saa 2 usiku na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) tarehe 03 Desemba, 2016.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya ngozi Dkt. Andrew Foi alisema mtoto Haidari anayeishi Mbagala Kuu Jijini Dar es Salaam alianza kuota nyama miezi mitatu baada ya kuzaliwa na amekuwa akifanyiwa upasuaji wa kuondoa nyama hizo mara kwa mara.

Dkt. Foi alisema Hospitali ya Taifa Muhimbili inatoa matibabu ya mtoto huyo bure tangu awasili hospitalini hapo isipokuwa kwa matibabu ambayo hayapatikani hospitalini hapo ndio analazimika kuyalipia katika sehemu husika.

Alisema mtoto Haidari anahitaji eneo maalum la kuishi muda wote ambalo lina giza na kuvaa nguo nyeusi zinazomfunika mwili wote ili kujikinga na miale ya jua ambayo imekuwa ikimuathiri kwa kiasi kikubwa.

Mama wa mtoto Haidari, Ndugu  Sauda Kassim alimshukuru Rais Dkt. Magufuli na mke wake Mama Janeth Magufuli kwa moyo wa upendo waliouonesha baada ya kuguswa na shida zinazomkabili mtoto wake na kutoa msaada huo na hivyo kuomba wananchi wengine waige mfano wa Rais na Mkewe katika kumsaidia mwanawe.

Tayari mtoto Haidari  Bonge, ameshafunguliwa akaunti katika Benki ya CRDB tawi la Azikiwe yenye namba 0152236450100, ambapo benki hiyo kupitia kwa meneja Uhusiano wake Godwin Semunyu amekabidhi shilingi laki Tano ikiwa ni msaada kutoka Benki hiyo.

Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam


Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts