Get the latest updates from us for free

Home » » Rais Magufuli Akutana Na Kufanya Mazungumzo Na Marais Mbalimbali Wa Afrika Katika Makao Makuu Ya Umoja Wa Afrika (Au) Mjini Addis Ababa Ethiopia

Rais Magufuli Akutana Na Kufanya Mazungumzo Na Marais Mbalimbali Wa Afrika Katika Makao Makuu Ya Umoja Wa Afrika (Au) Mjini Addis Ababa Ethiopia

Written By Bigie on Wednesday, February 1, 2017 | 12:38:00 PM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli,  jana Tarehe 31 Januari, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na Marais watatu wa Nchi za Afrika, Waziri Mkuu wa Ethiopia na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kando ya Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika uliomalizika leo Mjini Addis Ababa Nchini Ethiopia.

Mhe. Rais Magufuli amewaalika viongozi wote kuitembelea Tanzania ili wapate muda zaidi wa mazungumzo ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kwa lengo kukuza zaidi biashara, uwekezaji na kuboresha maisha ya wananchi.

Kwanza, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ambapo viongozi hao wamezungumzia miradi mbalimbali ya ushirikiano na fursa za biashara ambazo Tanzania na Uganda zinaweza kuzitumia kujiongezea mapato. Mhe. Rais Museven amekubali kufanya ziara nchini Tanzania katika siku za karibuni.

Pili, Mhe Rais Magufuli amekutana na Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Mhe. Abdel Fattah El-Sisi ambapo viongozi hao wamezungumzia namna nchi hizo zitakavyoshirikiana katika nyanja mbalimbali zikiwemo afya, kilimo, mifugo na viwanda.

Pamoja na kukubali mwaliko wa Rais Magufuli wa kufanya ziara rasmi nchini Tanzania, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi pia amekubali ombi la kuwaleta wataalamu na wawekezaji wa Misri nchini Tanzania ili wajenge viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba vya binadamu, kuinua teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji, kuwekeza katika viwanda vya nyama na viwanda vingine ambavyo nchi hiyo imepiga hatua kubwa.

“Mhe. Rais El-Sisi nakupongeza sana kwa juhudi zako za kuijenga Misri na nitafurahi sana kuona biashara ya Tanzania na Misri inaongezeka maradufu kwa manufaa ya pande zote mbili” amesisitiza Mhe. Dkt Magufuli.

Tatu, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Rais wa Afrika ya Kusini Mhe. Jacob Zuma ambapo pamoja na kukubali kufanya ziara rasmi nchini Tanzania, viongozi hao wamekubaliana kuwa baada ya kazi kubwa ya harakati za ukombozi nchi hizi sasa zina kila sababu ya kuelekeza nguvu katika kuongeza biashara na uwekezeji.

Nne, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Bw. Akinwumi Adesina ambapo pamoja na kumshukuru kwa ushirikiano mzuri ambao Tanzania inaupatakutoka Benki hiyo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, amemuomba kuendeleza na kuongeza zaidi ushirikiano huo hasa katika maeneo ya kipaumbele ambayo Tanzania inayatekeleza hivi sasa.

Kwa upande wake Bw. Akinwumi Adesina amesema Benki hiyoitaendeleza ushirikiano na uhusiano wake na Tanzania na kwamba Tanzania itanufaika kupitia vipaumbele vipya vya AfDB viitwavyo “Hi 5” vinavyohusisha uwezeshaji miradi ya uzalishaji wa nishati, ujenzi wa viwanda, uzalishaji wa chakula, miundombinu ya kuunganisha nchi na nchi na kuboresha maisha ya watu.

Pia Bw. Akinwumi Adesina amekubali ombi la Mhe. Rais Magufuli la kuitaka AfDB kushirikiana na Tanzania kupata suluhisho la kuzalisha umeme mwingi na wa gharama nafuu na ameahidi kumtuma Makamu wa Rais wa AfDB anayeshughulikia masuala ya nishati kuja Tanzania haraka iwezekanavyo ili kuanza utekelezaji wa ombi hilo.

Tano, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn na amemualika kufanya ziara rasmi nchini Tanzania ili wapate nafasi ya kuzungumza zaidi juu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo.

Pamoja na kukubali mwaliko wa Rais Magufuli, Mhe. Hailemariam Desalegn amempongeza kwa mabadiliko makubwa ya uchumi ambayo Serikali ya awamu ya tano inayafanya nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kukabiliana na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ambao Rais Magufuli amehudhuria kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani umemalizika jana Mjini Addis Ababa na Mhe. Rais Magufuli anatarajiwa kurejea nyumbani leo

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Addis Ababa


Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts