Home » , , » Mpenzi Wangu Ibilisi ( Simulizi ya Kweli) Sehemu ya 03

Mpenzi Wangu Ibilisi ( Simulizi ya Kweli) Sehemu ya 03

Written By Bigie on Saturday, February 24, 2018 | 2:44:00 PM

Mwandishi: Grace Godfrey Rweyemam

Nilifikiri kuwa kwa kesi yake, angehitaji mchungaji au mtumishi wa Mungu mwenye nguvu na uzoefu wa kushughulika na nguvu za giza na nguvu za kichawi. Akiendelea kuongea, akilini alinijia kaka yangu mmoja ambaye ni mchungaji, nikakumbuka katika uzoefu wake wa kuombea watu wanaosumbuliwa na mambo mbalimbali amewahi kukutana na kesi za mapepo na wachawi mara kadhaa. 

Lakini nilianza tena kuwaza kama muhusika angekubali habari yake aambiwe mtu mwingine yeyote. Mazungumzo yetu yalikuwa siri kubwa ambayo nina hakika hangetaka yajulikane kwa watu. Aliamua kuniamini mimi pekee, na kumjulisha mwingine kwake ilikuwa kama kuyaweka maisha yake hatarini.

Baada ya maongezi ya muda mrefu, huku nikimsikiliza neno kwa neno, nilianza kupangilia namna ya kumjibu. Nikachukua kama sekunde kadhaa nikitafakari, kisha nikamwambia, “Unaweza kuniamini?” Nilianza kwa kumuuliza, akanijibu ndio huku akionyesha kutafakari kwanini nimemuuliza hivyo. 

Niliisoma akili yake ikijiuliza inakuaje namuuliza swali kama hilo ilhali tayari ameniamini sana na ndio sababu ya kuja kuongea na mimi. Ni kweli aliniamini, lakini nilimtaka aniamini zaidi ya hapo. Nilimtaka aniamini kwa maamuzi niliyotaka kuyafanya, aamini kwamba nitamuweka kwenye mikono salama ya mtu atakayeweza kumsaidia zaidi yangu.

Nilianza kumueleza kwa kirefu kuhusiana na kaka yangu ambaye ndiye mtu nilifikiria angemsaidia. Unajua hata inapokuja kwenye suala kama ajira, kabla ya kumuunganisha muajiri kwa mtu anayetafuta kazi, ni vema ukahakikisha ameelewa na kukubali vigezo vya huyo ambaye unataka aajiriwe kwanza. Sasa hapa ilikuwa ni zaidi ya kazi ya kuajiriwa, bali mustakabadhi wa maisha ya mtu, ilikuwa ni muhimu sana kwamba nimuunganishe na mtu ambaye sitamfanya ajutie kujiweka wazi kwangu. 

Nilimueleza kwa kirefu sana uzoefu wangu juu ya huyu kaka, nikampa shuhuda kadhaa za namna ambavyo Mungu amekuwa akimtumia kuwahudumia watu mbalimbali. Kwa mfano kuna siku ambayo alitembelea shule fulani ya msingi ya bweni kwa kualikwa na mwalimu, ambapo akiwa tu anapishana na watoto, walikuwa wakianguka na mapepo, na watoto wengi sana walihudumiwa siku hiyo. Nikamwambia na shuhuda nyingine kadha wa kadha kuifanya akili yake iamini kuwa ni mtu ambaye anaweza akatoa msaada bora kuliko ambao mimi ningeutoa.

“Grace, ninaweza kukutana na huyo kaka yako?” Alianza kuniuliza kabla hata sijamwambia nia yangu ya kumuunganisha naye. Nilimkubalia na kumtafutia kukutana na huyo kaka yangu, akaenda nyumbani kwake. Alimuelezea pia kwa kirefu kwani nilihakikisha nimemtoa wasiwasi na kumjengea Imani juu ya huyo kaka yangu, hivyo akawa huru kujieleza kwake pia. Baada ya maongezi yao waliingia kwenye maombi, na hapo ndipo shughuli ilipofika mahala pake.

“Nilipoanza tu kumuombea mapepo yalilipuka, sasa mara nyingi huwa nikiwa pekeyangu napenda kuwarekodi watu ninaowaombea wanapoangushwa na mapepo,” alinieleza kaka siku niliyoonana naye, kisha akanipa simu yake niangalie ile video. 

Yeye hufanya hivyo ili kuwasaidia watu kujua jinsi gani shetani amewatesa, na ili wanapojitambua na kufunguliwa wajue nini hasa kilikuwa chanzo cha shida zinazowafunga. Nilimuona siyo yule Jovina niliyekutana naye, msichana mstaarabu na anayeongea kwa utaratibu sana. 

Alipopagawa na mapepo, alianguka chini kama mtu mwenye kifafa, akawa akigaagaa chini na kujitupa kwa nguvu. Nilikuwa nimemshauri awali kuwa siku atakayoenda kwa huyo kaka yangu mchungaji ni vema awe amevaa suruali, kwa ajili ya purukushani za maombezi. Yale mapepo yalimgalagaza chini kwa muda kisha mchungaji akayatuliza na kuanza kuyahoji. Yalijitambulisha kama jeshi la mapepo ya kichawi ya kike yanayoishi ndani ya yule binti Jovina.

“Alipokubali tu kuolewa na huyo mwanaume aliyenaye, alikubali sisi tuishi ndani yake. Kwa sasa bado hajakubali kuchukua nafasi katika chama chetu lakini huo ndio mkakati tulionao. 

Mume wake ni mtu mkubwa sana katika chama chetu, na anaheshimika duniani na kuzimu, hivyo ni lazima akamilishe heshima yake kwa kumsajili na mkewe. Hii ndiyo sababu hakutakiwa mke wake aishi kama mke wa tajiri, ili iwe rahisi pindi tutakapoanza kumshawishi ajiunge nasi na kuwa mshiriki wetu. Kwani mabinti wengi huwa na tamaa ya mali na sisi tunatumia hiyo fursa.

 Kwa sasa mkakati uliopo mezani nikumuua mwanae, lakini hilo ni jambo ambalo litamuumiza sana, hivyo endapo hatakuwa tayari kabisa, itabidi akubali kujiunga nasi mapema hii kumlinda mwanae.” Yalizungumza mapepo hayo kwa sauti kubwa yenye nguvu na ujasiri mwingi kiasi kwamba hungeweza kuhisi hiyo sauti inatokea kinywani mwa Jovina.

Kaka aliendelea kuyahoji kwa kirefu na yakatoa siri nyingi kuhusiana na yule mwanaume na siri za ndoa yake. Hakuwa amemwambia kuhusu jinsi ambavyo hawezi kupitisha hata usiku mmoja bila kufanya tendo la ndoa, lakini yale mapepo yalizungumza, “anadhani anampenda sana na kumtamani sana mume wake, lakini hajui kuwa ni sisi. Mara zote anayefanya mapenzi sio yeye, ni sisi ndani yake. Tunatembea na mumewe na ndio sababu hata afanyeje hawezi kumuacha.

 Hii inafanyika kwa mabinti wengi sana, wanakuwa na tamaa kwa wanaume, wengine hata sio waume zao. Pia tunawafanya wawe wazinifu na wasioweza kuzuia tamaa zao wakidhani udhaifu wa miili yao, kumbe ni sisi tunafanya kazi hiyo ndani yao. Wanajaribu kuturidhisha sisi kupitia miili yao, na kamwe hawaridhiki.”

Nikiangalia hiyo video nilianza kufikiri jinsi ambavyo shetani amewatesa watu kwa kuwaweka katika vifungo ambavyo hawawezi kujinasua. 

Nilikumbuka nimewahi kukutana na msichana ambaye kiukweli kwa sura, umbo na muonekano huwezi kumtoa kasoro, yaani ni binti mzuri mno. Lakini mwanamke huyu mdogo aliolewa na kudumu kwenye ndoa yake kwa miezi nane tu, kisha wakaachana na mumewe. 

Mume wake tunafahamiana kabla hajaoa, na aliponionyesha mwanamke anayemuoa, nilimpongeza kwa uzuri wa yule binti. Lakini mwaka mmoja na nusu baada ya ndoa yao tulionana akanieleza jinsi gani ndani ya miezi nane tu ya ndoa yao, alimfumania mkewe mara mbili, akaamua kumuacha, na hapo ni mbali na kubamba jumbe kadhaa za mapenzi kwenye simu yake.

Yale mapepo yalizungumza kitu kingine cha ajabu sana, nacho kikanifundisha kuwa wakati mwingine tunakuwa wepesi kufanya maamuzi tukitazama tu vinavyoonekana na kuvutia kwa macho. “Kabla mume wake hajamuoa, alishaoa wanawake watatu na hawakudumu kwa zaidi ya miaka miwili kwenye ndoa. 

Njia rahisi ya kuwapata wasichana wadogo ni kupitia pesa, hivyo watu wetu tunawapa pesa nyingi ili iwe rahisi kwao kushawishi wazazi wa mabinti. 

Kinachotokea ni kwamba baada tu ya kuoa, tunahakikisha aidha tunamuua huyo mwanamke ili kuongeza nguvu yetu kwa njia ya damu yake, au tunamfanya kuwa mmoja kati yetu na kumuondoa kumpeleka sehemu nyingine ya dunia. Huyu ndiye mwanamke pekee aliyeishi naye muda mrefu na ni kwa sababu sisi tumeona anaweza kuishi na sisi vizuri.”

ITAENDELEA 
#TrueStory

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts