Home » , » Mpenzi Wangu Ibilisi ( Simulizi ya Kweli) Sehemu ya 04

Mpenzi Wangu Ibilisi ( Simulizi ya Kweli) Sehemu ya 04

Written By Bigie on Sunday, February 25, 2018 | 3:34:00 PM

Mwandishi: Grace Godfrey Rweyemam
Baadaye mchungaji alianza kuyakemea na kuyawashia moto hayo mapepo, yakapiga kelele sana huku yakidai kuwa akiyafukuza yakaondoka mume wake hataweza tena kuishi. Yalidai kuwa kwa yeye kufanya maamuzi ya kwenda kuombewa ni kama kusababisha fedheha kubwa kwa mume wake na hivyo wakuu wake watamuua.

 Yalipiga kelele kwa nguvu yakidai kuungua kisha yakamtoka, nadhani wenye uzoefu wa kukemea mapepo mnanielewa. Nilizungumza na kaka yangu huyu mchungaji akanieleza baadhi ya vitu ambavyo Jovina hakuwa amenieleza kabla. 

Baada ya kufunguliwa alimwambia ukweli kuwa mara kadhaa amekuwa akiota kama katika kitanda chao wamelala yeye na mumewe na wanawake hata watatu au wane.

 Alidai hiyo hutokea mara nyingi sana, lakini pia alikiri kuwa licha ya kuwa yeye hufanya tendo la ndoa na mumewe kila siku, lakini siku zote amekuwa ni kama mtu ambaye ana muda mrefu sana hajakutana na mwanaume na hicho kitu kimemsumbua kwa muda mrefu sana. Yaani hali ya mwili wake kutamani mwanaume siku zote iko juu sana.

Siku hiyo baada ya kuombewa alidai hataki tena kwenda nyumbani kwake. “Sitaki tena kumuona mume wangu, simuhitaji tena, sijisikii kuwa naye na hii ni ajabu sana kwani mimi muda wote huwa najihisi kumtamani mume wangu. 

Hapa ninawawazia watoto wangu tu, lakini siko tayari tena kuishi nyumba moja na yule shetani tena. Hisia za mapenzi nilizokuwa nazo juu yake hazipo tena na simuoni tena kama mume wangu bali kama adui mkubwa,” Alieleza Jovina huku akisisitiza kutorudi tena nyumbani kwake. Niliwaza ni namna gani kaka yangu huyo mchungaji alitatua hilo, kwani alikuwa bado ni mke wa mtu na ana familia. Pia hapo akili ikaanza kujiuliza ni jinsi gani angerudi nyumbani kwake baada ya kumshambulia mume wake kiasi hicho katika ulimwengu wa roho.

“Ilibidi baada ya kufunguliwa, tufanye maombi ya ulinzi juu yake. Pia nilimuomba Roho mtakatifu atuongoze jambo sahihi la kuamua kwani ni kweli kurudi kwake nyumbani kulikuwa hatari kubwa na pia kutorudi kungesababisha hatari kwa watoto wake. Badae nilipata andiko la Biblia kunihakikishia kuwa ulindi wa Mungu uko juu yake, nikamuombea tu ulinzi na kumwambia asiogope, aende.” Alieleza kaka.

Siku ambayo Jovina alienda kukutana na kaka yangu mara ya kwanza alikuwa amenijulisha kabla, na siku hiyo waliyofanya maombi alinijulisha pia. Jioni akirudi kwake alinitumia ujumbe mfupi wa simu kuniambia, “Dada Grace nashukuru sana, tumefanya maombi leo na kaka, nimefunguliwa, ukionana naye atakuonyesha vitu vilivyokuwa vimenifunga. Pia ameniombea na kuruhusu nirudi kwangu japo sikuwa nataka”

Kesho yake nilipanga nimpigie simu mida ya mchana anieleze nini alikutana nacho nyumbani au mume wake kama alijua kuna vitu vimefanyika, lakini asubuhi sana alianza kunipigia simu yeye. Nilishangaa nikijua muda huo wangekua bado na mumewe nyumbani. Aliniambai mume wake ameondoka saa kumi alfajiri kwenda safari ya ghafla. Alidai tangu wafunge ndoa haijawahi kutokea safari ya bila taarifa. 

Akinieleza kiundani kuhusu jana yake alisema, “nimerudi nyumbani nimemkuta mume wangu sebuleni na watoto. Chakula kilikua tayari mezani, nikamsalimia lakini alijibu kiunyonge kama mgonjwa. Hakuniuliza nimetoka wapi wala chochote. Hakuwa mchangamfu kama alivyo siku zote na hakuonekana kutaka kujua chochote kuhusiana na siku hiyo tofauti na kawaida yake.

 Kikawaida mume wangu ni mtu rafiki sana hasa kwangu na tukiachana masaa kadhaa basi tuonanapo lazima anidodose kujua siku yangu ilikuaje, akiniuliza maswali ya hapa na pale na kunitania, lakini jana alikuwa tofauti kabisa. Nilipomkaribisha mezani kula hakuja na wala hakujibu kitu, nami nikaamua nimuache tu. Huwezi kuamini, kwa mara ya kwanza jana hajanigusa usiku na wala mimi sikujisikia kumtamani. 

Saa tisa alfajiri aliamka na kuniambia kuwa ana safari ya kikazi ya ghafla, akaanza kupanga nguo zake, saa kumi akaondoka. Sijamuuliza chochote, sijamlaumu na huu kwangu najua ni ushindi mkubwa. Mchungaji aliniambia sitakiwi kuogopa, Mungu ananilinda, ila sikuamini kuwa hatanifanya chochote na hata kuuliza, lakini sasa nimehakikisha kuwa kweli Mungu ananilinda.” Alinieleza Jovina, ila nilielewa vizuri hali halisi baada ya kuonana na kaka yangu siku kadhaa baadaye.

Mume wake Jovina alirudi wiki moja baadaye akiwa anaumwa. Mwanzo ilionekana ugonjwa wa kawaida tu, lakini siku chache zilizofuata alizidiwa sana. Hospitali hawakuona chochote kwenye vipimo, lakini hali ilizidi kuwa mbaya. 

Akiendelea kumuuguza mumewe, mwezi mmoja na siku chache baadaye, ndugu zake ambao siku zote hawakuwahi kuwa karibu naye walianza kudai apelekwe nje ya nchi kutibiwa.

 Ugonjwa alioumwa haukueleweka sana kwani alipungua uzito sana na kudhoofu, halafu ngozi yake ikaanza kama kubabuka na kuwa na rangi kama ya kijani. Baada ya kuzunguka hospitali zote kubwa hapa mjini, walimpeleka India, katika hospitali moja ya saratani wakihisi huenda ni saratani ya ngozi. 

Niliongea na Jovina kwenye simu akiwa India akimuuguza mumewe, akasema madaktari wanashangaa ni ugonjwa gani. Kuna dalili kadhaa zinaendana na ugonjwa wa saratani lakini vipimo vyote vya saratani vimekataa, saratani haionekani. 

Alidai kuwa tangu wamefika hapo madaktari wamekuwa wakimshughulikia lakini hali imezidi kuwa mbaya kwani anaumwa sana viungo vyote, ngozi inabadilika kuwa na rangi ya kijani, na sasa mwili umeanza kama kujaa maji baadhi ya maeneo.

 Kuna siku nyingine alinipigia simu akidai mumewe analia kwa maumivu kama mtoto mdogo kiasi cha yeye kumuhurumia na anatamani hata afe asiendelee kupata hayo mateso. Muda wote tangu alipoanza kuzidiwa hakuweza kuzungumza na ni kama pia hakuwa anaelewa hata mtu akizungumza naye, ila alihisi maumivu na mateso makali kwani alikuwa akilia sana.

Mume wa Jovita amefariki siku si nyingi, alifia India, wakamsafirisha na kumzika kifahari nchini Tanzania hapa jijini Dar es Salaam, makaburi ya kinondoni. Kwenye msiba wake walihudhuria watu wengi mno maarufu na matajiri, na ulikuwa msiba wa kifahari. Lakini najiuliza, imemfaidia nini ufahari wa msiba au wa maisha aliyoishi? Ni Dhahiri hakupata neema ya kutubu, kwani milango yake ya ufahamu ilifungwa mapema.

 Hii inanifundisha kuwa maisha tunayoishi tukiwa na nguvu na uzima huweza kutupa au kutukosesha neema siku zetu za mwisho. Mungu ni wa huruma, na nadhani huyo mwanaume angetubu, ingawa dhambi yake huonekana kuwa kubwa, angesamehewa. Lakini milango yake ilifungwa mapema, siyo kwa sababu ni mchawi, lakini ninaamini ni kwa sababu neema ilikuwa mbali naye.

Maisha tunayoishi tukiwa wazima hutengeneza hatima yetu ya baadaye. Hakuna ajuaye ni kifo cha namna gani atakufa, au ni siku ipi mwisho wake utafika.

 Usalama wa maisha ya mwanadamu uko ndani ya muumba wake na si vinginevyo. Huwa nafananisha maisha yetu na vyombo vya kuvunjika. Ni kweli bilauri inaweza kuwa nzuri sana na ya kuvutia, tena ikatumika nyakati maalumu tu ambazo wageni hutembelea nyumbani, lakini haina maana itaishi milele.

 Kuna siku hata bila idhini ya mmiliki wa bilauri hiyo huenda ikavunjika. Pengine ni mtoto ataipasua kwa bahati mbaya, au binti wa kazi akiwa anaiosha, au hata mwenye nayo huweza kuivunja bahati mbaya, na huo ndio ukawa mwisho wake. Siyo vifo vyote hupangwa na Mungu kama ambavyo wengine hudhani. Nakumbuka mstari kwenye Biblia unasema, Mungu hafurahishwi na kifo cha mwenye dhambi. Sidhani kama angekuwa anaua wenye dhambi ilhali hafurahishwi na vifo hivyo.

ITAENDELEA
#TrueStory

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts