Home » , » Mpenzi Wangu Ibilisi ( Simulizi ya Kweli) Sehemu ya 05

Mpenzi Wangu Ibilisi ( Simulizi ya Kweli) Sehemu ya 05

Written By Bigie on Monday, February 26, 2018 | 1:43:00 PM

Mwandishi: Grace Godfrey Rweyemam
Tukubali tukatae kuna adui wa kila mwanadamu, yaani ibilisi shetani. Huyu hana rafiki, hata kwa wanaompenda yeye si rafiki. Utamtumikia na kufanya mambo yake lakini mwisho wa siku hana pema pa kukupeleka zaidi ya jemanam ambayo yeye huishi huko. 

Na hata utatenda mapenzi yake lakini hakuwekei ulinzi au kukuzuilia usipate mabaya, badala yake yeye mwenyewe husababisha mabaya kwako. Mungu ni upendo, na ndani yake hamna chuki. Ni shauku yake kila mwanadamu aishi kwa mapenzi na makusudi yake ili afurahie upendo wake. 

Lakini alimuumba mtu kwa sura na mfano wake, hivyo ameweka utashi ndani yake. Utashi ambao mtu huwa nao ndio humpa nafasi ya kukubali au kukataa upendo wa Mungu, na hakuna namna ambayo Mungu huweza kutulazimisha tuwe vile anataka. Ameweka chaguo mbele yetu, uzima na mauti, uzima wa milele na mauti ya milele. Kwa anayechagua uzima akiwa hai huyo atauishi uzima huo hata baada ya kufa.

Najua kuna watu hawaamini kile ninachokiamini mimi, lakini hata wana sayansi huzungumza vile walivyothibitisha. Mwana historia anayesema binadamu wa kwanza aikuwa sokwe, ana vithibitisho vyake, ingawa yeye mwenyewe hakuwa sokwe kabla ya kuwa binadamu. 

Kwa miaka zaidi ya ishirini kama mkristo, na hasa katika uzoefu wangu wa Mungu kuniponya na uvimbe ndani ya ubongo wangu, na changamoto nilizopitia wakati huo hata kufikia hali ya kufa, nimehakikisha jambo moja juu ya kile ninachokiamini, kuwa ni kweli Mungu yupo na anaishi ndani ya wanadamu kwa njia ya Yesu Kristo na Roho mtakatifu. 

Ni Dhahiri kwa kila anayekubali na kumpokea Yesu, kama ambavyo ilitokea kwa Jovina, ndani yake hutokea badiliko la kweli la maisha. Haingekuwa rahisi binti huyu ambaye ndani ya miaka sita amekuwa chini ya kifungo cha mume mchawi kurudi nyumbani kwake kwa ujasiri huku akijua ameshaharibu kazi za mumewe. 

Kwake yale maombi hayakuwa tu muujiza wa mtoto wake kulindwa asiuliwe na mumewe kama ambavyo awali alidhani, bali yalikuwa maombi yenye badiliko kwa maisha yake kwa ujumla. Mchungaji alimuongoza maombi baada ya kumuelewesha kuhusu yeye binafsi kufanya uamuzi wa kumkubali Kristo.

Mara nyingi tumekutana na changamoto na tukaamua kumtafuta Mungu ili kupata suluhisho la changamoto zetu, lakini mtu anayenunua ndoo ya maji kuna siku yatamuishia, na ni bora kwake angechimba kisima. Kuwa na Kristo ni sawa na kisima cha maji yasiyokauka, na hicho ndicho ambacho kila mtu huhitaji. 

Yeye hangemsaidia Jovina kulinda mtoto wake tu, bali pia kuondoa hisia za mapenzi zilizowekwa kichawi ndani ya moyo wake, na halafu kumpa ujasiri dhidi ya mumewe ambaye mwanzo hakuwa na uwezo wa kukataa kile alichotaka. 

Zaidi sana hata kama mumewe angetaka kumuua baada ya yale maombezi, Mungu aliweka ulinzi juu yake, na tofauti na ambavyo mabinti wenzake walioolewa na huyo mwanaume kabla yake waliishia kuuawa au kuwa wachawi, Jovina sasa ni msichana huru na badala yake amekufa huyo mume wake.

Halijawa lengo langu kutangaza dini fulani, au kumtangaza kaka yangu huyo mchungaji, ndio sababu sijamtaja jina lake, lakini lengo langu nimtambulishe Kristo mioyoni mwa watu wote. Tunaishi kwenye dunia yenye hatari nyingi tusizoziona na nyingine tunaziona. 

Kati ya vitu amewahi kunieleza Jovina kuhusu mume wake ni jinsi ambavyo alikuwa akitaka kusababisha lolote kwa mtu yoyote hufanikiwa bila shida, endapo huyo mtu hana ulinzi wa Mungu juu yake. Mume wake aliwahi kumwambia kuwa asilimia kubwa sana ya wanadamu hutembea bila ulinzi wowote na kuna mambo mengi mno hutokea siyo kwa kawaida kama wanavyodhani, bali husababishwa na nguvu za giza. Kwa mfano, kuna wakati wachawi huamua kutengeneza magonjwa, halafu mtu akaenda hospitali na kupimwa na kukutwa na huo ugonjwa akadhani ni ugonjwa wa kawaida. 

Siyo kila saratani unayoiona ni seli za mwili zimepoteza uwezo wa kuzaliana kiasili, ingawa kuna nyingine ni kweli ni za asili. Hii niliithibitisha hata kabla sijakutana na Jovina, kaka yangu huyohuyo aliwahi mara kadhaa kuombea wagonjwa halafu wakati wa maombezi mapepo yanalipuka na kujieleza kuwa sisi tumesababisha saratani au UKIMWI ndani ya huyu mtu, na tunampa dalili kisha tunasababisha hospitali uonekane ni huo ugonjwa, lakini kimsingi siyo ugonjwa bali ni nguvu za giza ndani yake. 

Na ukifuatilia vizuri utagundua kweli ni siyo ugonjwa wa kawaida sana. Wakati mwingine unaweza ukaona labda kwa wale wanaofahamu, kiwango cha saratani kinasoma hatua ya nne ambayo kimsingi ni hatua mbaya na ya mwisho, lakini dalili zinaonekana kana kwamba ni hatua ya pili hivi. Pia mume wake huyo aliwahi kumwambia kuwa ajali nyingi mno husababishwa na wao, ili kusababisha vifo.

Ni vema na sahihi kabisa kupata msaada wa haraka wa matibabu tunapoumwa, lakini kazi ya madaktari ni kutibu tu, na siyo kuponya. Mara kadhaa nimekutana na kesi ambazo madaktari wamekiri wenyewe hawawezi kufanya chochote, lakini wahusika walipomruhusu Mungu awahudumie, wamepona kabisa. 

Mimi mwenyewe nikiwa shahidi, kwa waliofuatilia ushuhuda wangu wa JIPU NDANI YA UBONGO wanajua kuna sehemu ilifika madaktari walikiri kuwa kimsingi nimekufa, lakini Mungu ambaye ndiye chanzo cha uhai ndani yangu, alinirejesha, kwani wakati wangu haukua umefika bado. 

Hii haimaanishi kuwa ukikaa vema ndani ya Kristo hutakufa kwa magonjwa au kwa namna yoyote ile, lakini salama yako ni kwamba adui shetani anakosa mamlaka dhidi ya maisha yako na uhai wako. Hata wakati ambapo huruhusiwa kukugusa kama alivyonigusa mimi kwa kunisababishia uvimbe kwenye ubongo, bado Mungu hukupa mbinu sahihi za kumpinga, huku ulinzi wake ukiwa mkuu mno juu yako na hakuna chochote kinaweza kutokea endapo Mungu hajaruhusu.

Nina uhakika wa asilimia mia moja kuwa niko salama mikononi mwa Mungu. Nami najua kwa asilimia zote shetani hanipendi na angetamani kunimaliza leo hii. Najua kuna mitego kadhaa ya ajali, magonjwa na mambo mengi maovu ambayo hutega kwa ajili yangu, kama ambavyoo hutega kwa watu wengine wote ambao Mungu amewaumba kwa sura na mfano wake, lakini ukikaa vizuri ndani ya Kristo, ataishia kutega tu na hakuna anachoweza kusababisha. 

Roho mtakatifu ndani yangu hunijulisha aidha moja kwa moja au kwa njia yoyote ile juu ya mitego ambayo adui hutega kinyume nami, na hunipa neema ya kuomba, na kuweka ulinzi. Huu si upendeleo kwangu, na kama ingekuwa hivyo, nisingesema hivyo mbele ya watu wengine. Hii inawezekana kwa kila anayehitaji na kukubali. 

Jovina alichohitaji ni kukubali tu kile alichoshauriwa na mchungaji, na huo ndio ukawa mwanzo wa maisha yake mapya. Miaka yake sita ya hofu iliisha ndani ya siku moja, na mpaka sasa, licha ya kuwa mjane katika umri mdogo, Amani na furaha yake ni nyingi kuliko ilivyowahi kuwa kabla.

Watu walimuhurumia kwa kumpoteza mume wake, na kuna wengi ambao walikuwa wakiwaona kwa nje na kuwatamani jinsi ambavyo wanapendana, lakini hawakujua kifungo ambacho Jovina alikuwa nacho. Najua kuna wengi wanaosoma ambao hali zao hazina tofauti sana na huyu binti, japo siyo kwa kuwa na mahusiano na wachawi. Watu wakuonapo kwa nje huona binti au kijana aliyejaa fahari nyingi, huona mwanaume au mwanamke asiye na shida yoyote, lakini unajua moyoni mwako kuwa unaishi Jehanam ya duniani. 

Unajua mateso uliyonayo katika ndoa yako, malezi yako ya watoto, afya yako, uchumi wako au hali yoyote ile unayopitia au wanayopitia wapendwa wako. Unamuhitaji Mungu, unamuhitaji Yesu awe chemchem ya mema ndani yako. Ni bora kupitia katika hali ngumu ambayo Muumba wako ameiruhusu, kuliko kupita kwenye mateso yaliyosababishwa na shetani bila msaada wa Mungu. Ni kweli tunatafuta suluhisho kwa matatizo tunayopitia, lakini mara nyingi hatung’oi mizizi ya matatizo hayo, hivyo tunaendelea kuishi ndani ya vifungo vya mateso.

Zaidi sana mioyo yetu imejaa huzuni na sononeko. Tabasamu tunazozionyesha kwa nje machoni pa watu, siyo halisi kabisa. Hii si sahihi kabisa. Mungu alimuumba mwanadamu afurahie siku ambazo amepewa kuishi duniani. Utakubaliana na mimi kuwa kuna matajiri wengi huonekana kuwa na kila kitu lakini mioyo yao haina amani. Kila ambacho mtu huweza kuwa wacho, ni chema na bora zaidi ikiwa mahusiano yake na Mungu ni mazuri, sawa sawa kabisa na mtoto anavyokuwa salama mikononi mwa mzazi.
 
Kabla ya kuandika simulizi hii kumuhusu, Jovina alinifuata wiki iliyopita, alipoona nimeanza kutuma simulizi za kweli za maisha ya watu kwenye kurasa yangu. Kiukweli sikuwa na mpango wa kuandika simulizi yake kwani sikuwa na hakika kuwa atakuwa huru, hata kama nisingetumia jina lake, lakini bila mimi kumshawishi aliniomba ikiwa nitaweza niandike na kushea na wengine kuhusiana na maisha yake. Alidai jinsi ambavyo ameishi na mume wake na amemjua kwa ukaribu kama mchawi mwenye nguvu nyingi, ameelewa ni kiasi gani ulimwengu wa giza ni halisi, vile vile ulimwengu wa nuru.

“Tatizo ni kwamba katika ulimwengu wa giza, wachawi na mapepo hufanya mambo kwa uhalisia na kwa Imani kubwa sana. Wao hawana wasiwasi na nguvu zao, na hawachoki kujaribu wanapohitaji kufanya jambo. Yaani ukikuta mtu ni mchawi, kiuhalisia yeye hujitoa mzima mzima kuwa mtumishi wa shetani, na humtumikia bwana wake kwa jitihada, na hivyo kufanikiwa sana katika njia zake. Wakati huo sisi ambao tu watoto wa Mungu na tunadai tunampenda Mungu, hatujitoi vya kutosha. 

Maisha yetu ni kama hatuna uhakika na yule tunayemtumikia. Hatuna muda wa kuomba, kujifunza sheria za Mungu wala hata kufanya yale ambayo tunatakiwa kufanya kwa bidii. Hii ndiyo sababu ulimwengu wa nuru hauonekani kuwa na nguvu sana. Wachawi na mapepo yanawatesa watu bila kujali dini zao, lakini nguvu ya Mungu ni kubwa mno kuliko nguvu ya wachawi endapo tutaijua na kuitumia.” Alisema Jovita, akisisitiza umuhimu wa kuwambia watu kuhusiana yale aliyopitia. Nami namalizia simulizi hili la kweli kwa kumshukuru kuwa sehemu ya kugusa maisha ya watu kadha wa kadha kupitia maisha yake.

MWISHO....

==>Kesho kuna ushuhuda mwingine utawekwa. usikose kkutembelea

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts