Home » , » Kabla Sijafa - Sehemu ya 03( Simulizi ya Kweli)

Kabla Sijafa - Sehemu ya 03( Simulizi ya Kweli)

Written By Bigie on Saturday, March 3, 2018 | 9:06:00 AM

 Mwandishi: Grace G. Rweyemam
Nakumbuka kuna siku nikitoka kazini, kwa kutumia simu ya yule mwanamke, mumewe alinitafuta kwa jumbe za kwenye simu, akiniomba tuonane. Nilipofika sehemu ambayo tulikuwa tukionana, nilikuta wanaume watatu, wawili wakiwa mabaunsa. Walinichukua hapo na kunipeleka sehemu wakiwa wamenifumba macho, wakanifanyia vitendo vibaya na kuniacha. 

Nilichukua taxi na kurudi nyumbani nikiwa na aibu kubwa, hata sielewi nimueleze nini mke wangu. Unajua wanawake wana mioyo ya ajabu sana. Nilimdanganya kuwa watu walinivamia, wakanichukua na kunifanyia hivyo vitendo, akanihurumia sana, akalia sana. 

Nilikaa siku mbili siendi kazini, nikajihisi vibaya vile ambavyo mke wangu alionekana kunipenda na kunihurumia wakati nimefanyiwa vitendo hivyo kwa ajili ya kumsaliti. Niliamua kuwa nitaacha kabisa tabia ya kumsaliti mke wangu, tukakaa kama mwaka au miezi kumi nikijizuia, lakini bado kuna mara kadhaa tulikosana na kununiana.

Nikiwa nimechoshwa na ile hali, nilianza kuondoka nyumbani kila tukinuniana, nikaenda mtaani na kuchukua wanawake wa mtaani. Nilichukua machangudoa, huku nikijifariji kuwa ningetumia kinga, ila nia yangu ilikuwa tu kupata faraja. Kuna msichana mmoja niliwahi kumchukua katika hali hiyo, nikamalizana naye na kumpa pesa yake, lakini aliniomba tuendelee akidai amenipenda na hangependa tuishie hapo.

 Alidai hata kama mimi ni mume wa mtu, yuko tayari kuwa na mimi bila malipo, na endapo ningekubali kumpangishia tu chumba kimoja na kuwa nampa pesa kidogo ya matumizi, basi angeachana na uchangudoa na kuwa wangu peke yangu. Sikuwaza mara mbili kwakweli, nilimkubali, nikasema ningemjaribisha kwa mwezi hivi halafu nimfanyie anavyotaka.

Kweli ndani ya mwezi nilimpangishia chumba, tukaanza mahusiano rasmi akawa nyumba ndogo yangu. Kwake nilipata kila kitu kama nilivyotaka, na hata siku moja hakuwahi kuninunia. Alinifanya kama mtoto mdogo nilipofika kwake, yaani kunibembeleza na kunihudumia mpaka kunivua soksi, akanifanya nimuone mke wangu takataka. 

Kwa bahati nilipata nafasi mpya kazini, yenye pesa nyingi na safari za mara kwa mara. Nikawa nikisafiri naye kila inapotokea safari ya kikazi. Nilianza kuona maisha yangu yamenyooka, na sina tena msongo wa mawazo kwani mke wangu hakuwa ananibabaisha tena.

Nilisahau tulipoanzia na mke wangu, nikasahau alivyonipenda kama mwanaume wake wa kwanza na wa pekee kabisa. Nilisahau jinsi ambavyo mwaka wa kwanza wa ndoa yetu, tukiwa tunatafuta mtoto, niligundulika nina tatizo la nguvu za kiume na huenda sitaweza kuzaa. Mke wangu wakati huo alikuwa na kazi nzuri sana, na kwa bahati mbaya sikupata kazi haraka baada ya mkataba wangu wa kazi ya kwanza kuisha, hivyo sikuwa na kazi kipindi hicho. Mke wangu alinigharimia kwenda nchi za nje, tukaonana na wataalamu zaidi, wakatusaidia, tukapata mtoto. 

Pia nakumbuka siku niliyojua kuwa nina tatizo, nilichanganyikiwa sana, lakini Marietha mke wangu alikuwa faraja kubwa kwangu akinihakikishia kuwa kamwe hangeweza kuniacha hata kama hatungepata mtoto maisha yetu yote. Marietha hakunipenda sababu ya pesa, kwani tulianza mahusiano nikiwa mwaka wa pili chuo na yeye mwaka wa kwanza.

 Familia yao ilikuwa yenye uchumi wa juu, na Marietha alikuwa tayari sana kutoa pesa zake kwa ajili ya mahitaji yangu mara zote. Pia siku zote tukiwa kwenye ndoa alihakikisha ninakula na kuvaa vizuri, licha ya kuwa ni mwanamke msomi na mwenye pesa. 

Ingawa aliajiri wafanyakazi wa kumsaidia, lakini hakuwa mwanamke asiye wajibika. Alisimamia na kuhakikisha kila siku nguo zangu zimefuliwa na kunyooshwa, nyumba ni safi, chakula kipo mezani kwa wakati na ni kizuri.

Siku ya siku niligundua kuwa yule mwanamke wangu kimada ana mwanaume mwingine, nikakasirika sana, na hapo nikaamini kuwa wanawake si waaminifu, hivyo nikasema sitakuwa na mchepuko mmoja. Niliamua kuwa nitakuwa na wanawake wengine mbalimbali, yaani kila anayenivutia nitamshawishi, niingie naye kwenye mahusiano. Nilipotaka kumuacha, alinibembeleza, tukaendelea naye, lakini wakati huo nikiwa tayari na mwanamke mwingine. 

Kama miezi miwili mbele, tuligombana tena na yule kimada, nikakusudia kumuacha, wakati tunarushiana maneno, akaniambia kuwa hata nikimuacha tayari ameshanipa la kufa nalo. Nilitamani anachosema kiwe sicho nilichoelewa, hivyo sikumlazimisha afafanue zaidi. Nilimuuliza tu ana maana gani, akanijibu nijaze mwenyewe, nikamuacha. Nilianza kuwaza sana, nikihisi kabisa kuwa alimaanisha UKIMWI. 

Niliamua nijikaze niende nikapime. Kile kimuhemuhe nilichopata siku ile, endapo ningekuwa sijaathirika, nadhani ule ndio ungekuwa mwisho wangu wa kutoka nje ya ndoa. Kwa bahati mbaya tayari nilikuwa nimeathirika. Siku hyo nimepokea majibu nililia sana, nikawaza sana, nikajilaumu na kujihurumia sana, ila nikamuhurumia zaidi mke wangu asiye na hatia, pamoja na wanangu.

Nilikaa mwenye mawazo zaidi ya mwezi, nikajizuia nisimwambie mke wangu. Katika msongo wa mawazo, niliiambia nafsi yangu kuwa tayari nimeshaathirika, sasa ni bora nile raha tu. Nilikusudia kuwa kila mwanamke nitakayemtamani nitafanya naye mapenzi, bila kujali hata umri wake.
 
Ndani ya kipindi cha miaka kadhaa tangu nimegundua kuwa nimeathirika, nimeshatembea na wanawake ambao siwezi kutaja idadi yake. Nimetembea na wanafunzi wengi sana hasa wa vyuo vikuu, wake za watu, watoto wa shule za sekondari, machangudoa, na hadi wanawake walionizidi umri yaani mashuga mami. Nimeambukiza UKIMWI wanawake wengi, na kwa bahati mbaya sana wanawake wana nafasi kubwa ya kuambukizwa wafanyapo ngono na mtu aliyeathirika kuliko wanaume. 

Nakumbuka kuna wakati nilitembea na mabinti halafu nikaanza kuwaonea huruma baadaye, nikijilaumu kwanini ninawaharibia maisha, ila sikuacha kuendelea kuharibu maisha ya wasichana wengi kadiri nilivyoweza. 

Kuna ambao walikuja kugundua nimewaambukiza baada ya muda, wakawa wakinifuata na kunilaumu sana, nikajifanya nina roho ngumu, nisionyeshe kujali, ila kiukweli niliumia sana. Kilichoniumiza zaidi ni mara kadhaa nilizopata wasichana ambao ni mabikra, wakakubali kutoa bikira zao kwangu.
 
ITAENDELEA KESHO
#TrueStory

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts