Home » , » Kabla Sijafa - Sehemu ya 04( Simulizi ya Kweli)

Kabla Sijafa - Sehemu ya 04( Simulizi ya Kweli)

Written By Bigie on Sunday, March 4, 2018 | 9:09:00 AM

Mwandishi: Grace G. Rweyemam

Siwezi kuelezea majuto niliyonayo leo hii. Dhambi niliyotenda inastahili adhabu. Mke wangu aliwahi kunionya mara kadhaa kuwa ana wasiwasi na mwenendo wangu na haniamini tena, akanionya nisije kumletea UKIMWI, bila kujua kuwa tayari ni muathirika. 

Ingawa aliwahi kupata tetesi kuwa mumewe si muaminifu, lakini kila alipotafuta kujua undani sikumpa hiyo fursa. Sikuwahi kuruhusu akutane na jumbe za mapenzi kwenye simu yangu, wala sikuwahi kuruhusu apigiwe simu na mwanamke mwenzie. 

Sikutamani ajue tabia zangu, ingawa muda ulivyozdi kwenda na nilipoanza kuwa na wanawake wengi alijua kabisa ndoa yetu iko matatani, mpaka kuna siku akadai nafsi yake inamwambia kuwa ninamsaliti na hivyo hana amani hata kuendelea kushiriki na mimi tendo la ndoa. 

Kuna wakati alijaribu kujitenga na mimi lakini alikuwa tayari amechelewa, kwani nilishamuambukiza wakati huo. Tulitengana na mke wangu chumba kwa miezi kadhaa, huku nikiwa tayari najua mimi ni muathirika wa muda mrefu, ila sikumwambia mpaka kipindi nilipoanza kuumwa.

Nilijitahidi kuwahi kutumia dawa lakini ni kama Mungu aliamua kunilipa kwa matendo yangu, kwani nilianza kuumwa ghafla na nikawa naumwa sana kana kwamba situmii dawa za kuongeza CD4. 

Pia nadhani kwakua nilikuwa nikitembea na wanawake wengi, nilipoteza nguvu nyingi sana, hivyo kunisababishia mashambulizi kuja kwa kasi. Mke wangu ana huruma sana, nilipoanza kuumwa alinihudumia kwa upendo, sasa kukawa hamna namna zaidi ya kukubali ajue ukweli, kwani ilikuwa lazima twende hospitali, na yeye ndiye angefuatilia vipimo. 

Ilibidi nijihami kumwambia ukweli kabla ya vipimo, nikamkalisha chini na kuanzia mbali sana, kisha nikasema ukweli kwamba nimeathirika, na huenda nayeye nimemuambukiza.

Sijasahau na kamwe sitasahau hisia ambazo Marietha wangu alizionyesha nikimpa taarifa hiyo. Alikuwa chumbani kwangu, mimi nimejilaza kitandani naye amekaa pembeni kitandani. 

Nilipoanza kumwambia, kabla sijamaliza, alianza kuhisi ninachotaka kusema, akahamaki sana. Alishuka kwenye kitanda akakaa chini, nikatamani nisiendelee kusema ila nikajikaza. Jasho jembamba lilimtoka japo kulikuwa na kiyoyosi. 

Alinyoosha miguu akiwa pale chini, akaweka mikono kichwani, halafu nikaona machozi yameanza kumtoka akiwa amenitazama kama mtu anayetaka niseme nilikuwa namtania.

Sikuwa na cha kujitetea, na wala sikuwa na namna ya kumuomba msamaha. Mke wangu hakusema chochote kwa wakati huo, akainuka na kwenda kujifungia chumbani. Alikaa muda mrefu sana chumbani kiasi cha kuniogopesha kuwa huenda akajidhuru. 

Nilijaribu kumgongea lakini hakufungua, watoto pia wakamgongea, nikawazuia, wamuache amepumzika. Usiku kabisa alitoka akaja tena chumbani kwangu, siku hiyo hata hakuwaaga watoto wakienda kulala.

 Aliniambia maneno machache, akalia kwa uchungu mno mbele yangu. “Ingekuwa rahisi kukusamehe kama ungekatisha ndoto zangu peke yangu, lakini umekatisha ndoto za watoto wangu. Unasababisha wanangu wakue bila wazazi. 

Unasababisha wanangu wawe yatima katika umri mdogo, na sijui ni nani anaweza kuchukua nafasi yangu kwao nikiondoka. Ni bora nisingezaa, ni bora ulipoona unashindwa kuwa mwaminifu ungeniacha, nikalea watoto wangu. 

Naumia nikiwaza wazazi wangu, kwani nina hakika mimi ni kati ya watoto waliowaamini sana. Kwa ulichonifanyia, Mungu atakulipa.” Alimaliza kuongea, halafu akaendelea tena kulia sana, kwa kwikwi. Macho yalikuwa yamemvimba, akionekana mtu aliyelia kwa masaa mengi kabla. 

Nafsi yangu haikuweza kustahimili machozi ya mke wangu, ila sikuwa na ujasiri wa kumbembeleza. Nilikuwa naumia sana, machozi yakinitoka pia, na niliumizwa zaidi na majuto yaliyokuwa ndani yangu.

Kesho yake alienda kupima akaonekana ameathirika pia, akaja na majibu na kunirushia, hakusema chochote nami pia sikusema kitu. 

Alimaliza siku kadhaa akiwa hazungumzi na mimi na akiwa mtu mwenye huzuni sana, ila baadaye nilianza kuzidiwa. Mke wangu alinihurumia na kuanza kwa upya kunihudumia kana kwamba hakuwa na kinyongo, ila hakuwa mtu mwenye furaha. 

Nilianza kuumwa kwa kasi sana, nikaongezewa kiasi cha dozi, nikashauriwa kuhusu vyakula, Marietha akawa akihakikisha nimekula vizuri. Nilikuwa nikipata nafuu kidogo lakini muda mwingi nilikuwa ni mdhaifu sana, nikajua nitakufa mapema.
 
Kwa sasa, ninajua kwa hakika sina siku nyingi za kuishi, na ndani ya nafsi yangu nimeshindwa kujisamehe, kwa kumkosea mke wangu, kwa kuwakosea wanangu na kwa mabinti na wanawake wengi mno wasio na hatia niliowaua. Ninaumia, moyo wangu unavuja damu. 

Nami nimeamua kabla sijafa niandike huu kama wosia wangu kwa watu wote watakaoweza kusoma au kusomewa. 

Najua ni aibu kubwa, ila natamani wosia huu usomwe siku yangu ya mazishi, ili kila atakayehudhuria, ajue ni kiasi gani huu ugonjwa huwatesa sio tu wanaousababisha, bali zaidi wale wapendwa wetu ambao walikuwa tayari kutoa mioyo yao kwetu na kuwa waaminifu katika ndoa zao. Mbaya zaidi huacha vizazi ambavyo bado vina uhitaji mkubwa wa kulelewa na wazazi.

Watu wengi hudhani kwamba wako salama, kwani kuna ile hisia kwamba ‘mimi haiwezekani.’ Mimi ni kati ya watu walioamini kwa zaidi ya asilimia mia kwamba haiwezekani kabisa nikapata UKIMWI. 

Haikuwahi kuingia akilini hata kidogo. Ujanani, kabla sijaoa na miaka ya mwanzo ya ndoa yangu nilikuwa mwaminifu mno, na sikuwahi hata kumpa mwanamke mmoja fursa ya kumuonyesha amenivutia, tangu nilipokuwa na Marietha wangu, lakini kitendo cha kuanza kufikiri kwamba ninaweza kupata faraja kwa mwanamke mwingine, ilikuwa ni sumu ya kufisha kwenye ndoa na maisha yangu yote kwa ujumla. Najua Marietha atausoma au kuusikia huu wosia, nami naamini ndani ya nafsi yake kuna siku atatoa nafasi ya kunisamehe, hata kama itamchukua muda.

ITAENDELEA KESHO
#TrueStory 

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts