Home » , » Kabla Sijafa - Sehemu ya 05( Simulizi ya Kweli)

Kabla Sijafa - Sehemu ya 05( Simulizi ya Kweli)

Written By Bigie on Monday, March 5, 2018 | 8:11:00 AM

Mwandishi: Grace G. Rweyemam

Nilikupenda Marietha mke wangu, kwa moyo wangu wote, na hakuwahi kutokea mwanamke bora zaidi yako, ila niliufumba ufahamu wangu kuona uzuri wa moyo wako pindi uliponikosea.

 Asilimia ishirini nilizokosa kwako zilinifanya kusahau asilimia themanini ulizonipa, za upendo na uzuri wa moyo wako. Nilisahau kuwa mara nyingi nimekuwa nikikukosea, ukanisamehe bure kabisa. Nilipoumizwa uliponinunia, nilitafuta kukukomoa, lakini sikujua ninatengeneza bomu la kuilipua familia yangu yote. Umenifundisha upendo wa kweli ni nini, lakini sikukubali kushika agano nililoliweka mbele ya Mungu na watu.

Sitamani mwanaume yeyote, na wala mwanamke, afanye kosa nililofanya au linalofanana na hilo. Ni vema kuzungumza na kutafuta muafaka unapokosewa au unapokosana na mwenzako, kuliko kutafuta amani kwingine popote. 

Wenzi tulionao ni wazuri, ila madhaifu yao kidogo hufumba macho yetu tusione uzuri wao. Maana halisi ya ndoa ni kumkubali mwenzi wako, kumpenda, na kuwa mwaminifu kwake, hata wakati ambapo unahisi amekuudhi. 

Uaminifu ni ngao kubwa mno kwa ndoa imara. Ninaomba unisamehe mke wangu, kwa kuyajua haya yote nikiwa nimechelewa kabisa. Natamani dawa ya UKIMWI igundulike ya kumtibu mtu mmoja tu, na mtu huyo awe wewe malkia wangu.

Nisamehe kwa kukunyima haki yako ya kuwa mama mpaka uzee wako, nisamehe kwa kukupunguzia miaka ya kuishi, nisamehe kwa kukatiza ndoto zako, nisamehe kwa kukatiza miaka yangu ya kuwa baba kwa watoto wako, nisamehe kwa kuwafanya wanao kuwa yatima kabla ya wakati, nisamehe kwa kuuumiza moyo wako na kuvunja imani uliyonipa, nisamehe hata kwa kuja kwenye maisha yako, kwani usingekubali kuolewa na mimi leo hii ungekuwa mwanamke mwenye furaha zaidi na maisha marefu.”Alimalizia.

Hii ni barua ya kwanza nimewahi kukutana nayo imeandikwa na marehemu, tena aliyejua anakwenda kufa. Ni kati ya vitu ambavyo kibinafsi vimewahi kugusa maisha yangu sana. Bahati alisema ya moyoni mwake, nadhani ilikuwa njia rahisi ya kujisamehe. Sijui kama alifanikiwa kujisamehe au la, ila zaidi natumai alikumbuka kutubu mbele za Mungu, kwa ajili ya kule aendako. Hilo anajua yeye na Mungu wake. Lakini kuna kitu ningependa kusema, hasa kuhusiana na maisha ya marehemu Bahati. 

Kuna binti aliwahi kutuma video moja kwenye mitandao ya kijamii, akieleza jinsi ambavo mama yake alimshauri baada ya kumlalamikia kuwa mume wake anatoka nje ya ndoa. Mama yake alisema kwamba wanaume ni sawasawa na mbuzi, beberu, ambaye huwekwa katika banda moja na mbuzi jike sita au zaidi, na huwabebesha mimba wote. 

Alimshauri kwamba hatakiwi kumfuatilia mumewe, anachotakiwa kujua ni kwamba hata kama anatoka nje, anapaswa amuheshimu tu na kutimiza majukumu yake. Mara kadhaa pia nimesikia watu wakisema, hakuna mwanaume mwaminifu, wanaume wote ni sawa, wanaume wote ni mbwa, na maneno ya namna hiyo.

Huwa najiuliza, kwanini Mungu amuumbe mwanaume asiyeweza kuwa mwaminifu kwa mke wake, halafu ampe masharti ya kutozini? Kwanini uzinzi iwe ni dhambi kwa mwanaume na mwanamke, endapo Mungu alimuumba mwanaume akijua hawezi kuwa mwaminifu kwa mwanamke mmoja? Hii hainiingii akilini. 

Ninashawishika kuamini kuwa wanaume au hata wanawake wanaozini, huaminisha akili zao kwanza kwamba ni jambo la kawaida na la kukubalika. Hata kama mke wako ni kimeo, au mume wako ni kimeo, kama ndani yako Roho wa Mungu anaishi, Yeye atakutenga mbali na dhambi, hasa ya uzinzi. Tatizo ni kwamba huwa tunatoa nafasi kwa dhambi kwenye akili zetu, halafu tunazitengenezea mazingira, kisha tunamsingizia shetani au kusingizia udhaifu wa wenzi wetu.

Sidhani kama njia sahihi ya kumuwajibisha mke asiyewajibika ni kwa kutoka nje ya ndoa. Sidhani kama ni sahihi kulipa kisasi kwa kuwa na mpenzi mwingine, mbali na mke au mume wako.
 
Hii dhambi imekaa sehemu mbaya sana, na inaangamiza familia, kama si kwa magonjwa kama UKIMWI, basi huua uaminifu, upendo na amani kwa familia nyingi, na kusababisha hata watoto kukua bila upendo wa kifamilia. Watu wengi wameishi tu kama wapangaji wenza na wakati ni mke na mume. 

Ni rahisi kusamehe makosa mengine mengi ya mwenzi wako, endapo ni mwaminifu kwako. Mwanaume au mwaanmke asiye mwaminifu, anapanda mbegu ya miiba, itakayoota na kumchoma yeye mwenyewe pamoja na wale awapendao. Tena hupika chakula cha sumu na kujitengea mezani yeye pamoja na familia yake.

 Natamani ifike mahala, suala la uaminifu katika ndoa liwe ni jambo la kawaida kwa kila wanandoa. Tunahitaji kubadili mtazamo, kwa wanawake na wanaume pia. Tunahitaji kuziaminisha akili zetu kuwa uaminifu ni lazima, na sio kitu hata cha kupongezwa. Ukiona unashindwa kuwa mwaminifu kwa mkeo au kwa mumeo, kwa sababu yoyote ile, nina wachungaji wanaoweza kukusaidia kiroho, kwani eneo hilo shetani amekaa na anakutafutia sababu ili akumalize, nitafute nikuunganishe nao.

Kwa ambao bado hawajaoa au kuolewa, nisingependa kuzungumzia sana, lakini nadhani wosia wa Bahati umewafundisha kitu kikubwa. Ni vema kufikiri uthamani wa ndoto na malengo uliyonayo, ambao ninaamini kabisa haulingani na starehe ya muda mfupi. Kuna vijana wengi, wenye nguvu na wanaokutana na vishawishi kama wewe, ambao hushinda kila siku, hivyo inawezekana kushinda, hasa ukikubali yeye aliyeuumba mwili wako awe kiongozi wa maisha yako.

Mwisho nizungumze na wanawake au hata wanaume wenye tabia za kununa, au tabia yoyote ambayo inaweza ikawa kero kwa mwenzi wako. Wenzi wetu ni wanadamu, na tunapowachosha na tabia zetu, tunatoa milango kwa mambo ambayo ni sumu kwa ndoa zetu. 

Ni bora kujifunza kusuluhisha kutoelewana kati yenu na si kuamua kununa. Ni lazima tujifunze kuwa wazi, kuzungumza, na kuziba kila upenyo ambao shetani huweza kutumia kuingilia mahusiano ya ndoa. Mambo tunayoyaona ni madogo huweza kuwa na madhara makubwa sana, tukiyapuuza.

MWISHO
#TrueStory  

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts