Home » , » Nguvu ya Dhaifu - Sehemu ya 01( Simulizi ya Kweli)

Nguvu ya Dhaifu - Sehemu ya 01( Simulizi ya Kweli)

Written By Bigie on Tuesday, March 6, 2018 | 12:33:00 PM

Mwandishi: Grace G. Rweyemam  

“Mamaaa”
Aliniita Kareen kwa sauti ya kustua sana. Ndani ya sekunde chache akili iliwaza mambo kama kumi hivi kwa hofu. Geofrey mume wangu akanitazama, “Usiwe unastuka sana, kelele kwa watoto ni kawaida.” Nilimpuuza na kuinuka mbio kuelekea kule nje walikokuwa wanacheza watoto. Ni kawaida kwa mtoto kuita hivyo, lakini sijui kwanini siku hiyo nilistuka sana. Ni kama nafsi yangu ilijua kuna kitu kimetokea. Ni kweli kuna kitu kilikua kimetokea, tena kitu kikubwa haswaa.

Baada ya ndoa sikupata mtoto mara moja. Niliolewa umri ukiwa umeenda kidogo tofauti labda na rafiki zangu wengi au ndugu zangu wengine. 

Ingawa mimi sikuona kama ni jambo baya au huenda sikujiona nimechelewa sana, ila kutokana na walionizunguka nilihisi nitatakiwa kupata mtoto mara tu nitakapoingia kwenye ndoa. Unajua mara nyingi matatizo tunayokuwa nayo katika maisha huwa hasa matatizo kwa ajili ya jamii inayotuzunguka. 

Yaani mfano mtu anayemaliza shule akakutana na changamoto ya kupata kazi, wanaomzunguka humfanya aione ni changamoto ngumu zaidi, hasa kwa maswali ya hapa na pale, mara, “Siku hizi uko wapi? Hivi kazi ulishapata? Kazi unafanyia wapi?” na maswali ya namna hiyo bila kujua kuwa unayemuuliza ana kazi au la, au ameshafanya jitihada gani za kutafuta kazi bila mafanikio. 

Au yale maswali ya una watoto wangapi? Au, bado hujazaa tu? Kwa mtu aliye kwenye ndoa, bila kujali ni kiasi gani anahitaji kupata mtoto.

Mimi nakumbuka kuna mtu, tena rafiki yangu, aliwahi kuniuliza, “unakawia hivyo kuolewa, unataka uje kuzaa mjukuu? Yaani nilishindwa kumuelewa, ni kwamba mimi najioa mwenyewe au ninakataa wachumba! Mwingine nikiwa na mwaka tu kwenye ndoa aliwahi kuniambia kuwa kama nashindwa kupata ujauzito nimwambie anisaidie, pengine mume wangu ana tatizo. Huyo aliyesema hivyo ni mwanaume, na alizungumza akimaanisha kwamba anisaidie kunipa ujauzito.

Sijui kama unaelewa ukiingia kwenye ndoa na presha ya kupata mtoto haraka, miaka mitatu bila mtoto wala mimba inakua mingi kiasi gani. Yaani kuna wakati mpaka nilikuwa nahisi hata nikitembea barabarani kila mtu anajua mimi ni tasa na hivyo naona aibu. Namshukuru sana Mungu mume wangu hakuwahi kuniumiza wakati huo. Wanasema ndoa huwa zina changamoto ya mapenzi lakini mimi hilo sikuwahi kujua. 

Mume wangu alinipenda kupita kiasi, na mpaka leo namshukuru Mungu sana kuwa niliolewa na mwanaume anayenipenda kwani changamoto nilizopitia kabla na baada ya kuzaa zingeniwia ngumu mno kama mume wangu angekuwa asiyejua kunionyesha upendo.

Tulibahatika kupata watoto mapacha baada ya miaka minne ya ndoa, yaani nikiwa na miaka mitatu na miezi minne nilibeba ujauzito na hivyo kujifungua mwaka wa nne mwezi wa kwanza. Mungu alikua ameamua kunifuta machozi yangu kwa kunipatia mara mbili ya kile nilichotamani. 

Sikuwahi kulala nikaota watoto mapacha kwa kweli, na wala kwenye ukoo wangu wala wa mume wangu hakuna mapacha. Tuliwaita binti zetu Kareen na Karitta. Binafsi ni mpenzi sana wa watoto wa kike tangu usichana wangu. Nilikua nikitamani sana watoto wa kike kwa sababu napenda mambo ya urembo. 

Yaani kichwani nilikuwa naona jinsi gani binti yangu nitamfanya kama ua la waridi kwa jinsi nitakavyomvalisha na kumpamba kwa mavazi. Hata madukani mara zote nguo za watoto wa kike zilichanganya kabisa akili yangu, kabla hata sijaolewa. 

Sasa nafikiri unanielewa ni furaha kiasi gani nilipata kupata mapacha wa kike, tena wanaofanana. Hapo nilijiona nina kila kitu, yaani nafsini sina sababu hata moja ya kuwa na huzuni. Nina mume ananipenda sana, uchumi wetu ni mzuri, tunaweza kufanya tunachotamani na sasa nina mabinti wawili warembo wanaofanana sana.

Mimi na mume wangu ni wakristo na tunampenda Mungu. Tumeoana kanisani, na hatukuwa na changamoto yoyote ya kimahusiano. Yaani Geofrey hajawahi kuniudhi kwakweli, kama amewahi ni makossa madogo mno, na kwa sababu ananipenda sana nadhani hata sio rahisi chochote anachonikosea kikae akilini mwangu hata nusu saa. Tofauti na wanaume wengi, Geofrey ni mwepesi mno kuomba msamaha na yeye hupenda sana amani. 

Tukiwa katika changamoto ya kutafuta uzao, hakuwahi kunionyesha kwamba tatizo lipo kwangu, japo hivyo ndivyo hospitali tuliambiwa. Kipindi cha nyuma nimewahi kuumizwa mara kadhaa na mahusiano hivyo imani yangu kwa Geofrey ilikuwa ndogo sana. 

Alipata kazi kubwa mno kunifanya nimuamini, na mpaka anafikia kunioa kiukweli bado sikuwa nimempa moyo wangu wote. Licha ya kuwa tulimpenda Mungu na Geofrey alinionyesha msimamo wake wa kiroho, lakini nilihisi tu ameficha makucha yake, ipo siku atanibadilikia. Nilikubali tu kuolewa naye kwa sababu ndiye mwanaume pekee niliyehisi ni bora kuliko wengine wote na umri wangu ulikuwa umeenda, hivyo nikaona kupunguza maneno ya watu ni vyema nimkubali.
 
Wakati naolewa nilikuwa na miaka kadhaa ya ukristo nikiwa nimeokoka, na maisha yangu hayakuwa na mambo mengi sana. Kwa asili yangu mimi ni mchangamfu na mcheshi kiasi hivyo huzoeana na watu kwa haraka. 

Kanisa nililosali nilikuwa na marafiki wengi na watu kibao nimezoeana nao, kiasi cha kuhisi kuwakosa pindi nilipotaka kuolewa. Ingawa mimi na Geofrey hatukuwa dini tofauti ila makanisa tuliyosali ni tofauti na kama mwanamke ilinilazimu kuhama kanisa kumfuata, kwani pia yeye kanisani kwake hakutaka kabisa kuhama. Kwangu hilo jambo sikuona ni gumu, tukaoana na kuanza maisha.

Maneno kadhaa yalisemwa kuhusiana na kuchelewa kupata watoto, mume wangu akawa akinikumbatia na kunituliza kila nilipolia, halafu aliniambia, “Angel, watoto ni zawadi tu, Mungu akiona jukumu la kulea linatufaa, atatupatia. Relax.” Mara zote alisema hiyo sentensi. Yeye si mtu wa maombi sana kama mimi, lakini ana imani yenye utulivu mkubwa ndani yake. 

Yaani nina hakika kama tusingebahatika kupata watoto kabisa, kwake haingekuwa tatizo kubwa, ila kwangu ndio sikuwa naelewa hata kidogo. Mimi ni wale watu ambao huwa hawampi Mungu pumzi juu ya jambo fulani. Nikitaka Mungu afanye kitu basi nitampigia kelele mpaka afanye. Nadhani Mungu huwa ananiona kama mtoto asije na uvumilivu. 

Nakumbuka mara nyingi nililia kila nilipoona damu ya mwezi, Geof akanikumbatia na kunifariji kwa maneno yake, nikaliaaa, halafu niliponyamaza nilienda kuomba na usiku huo ningeomba hata kwa masaa matatu au zaidi mfululizo juu ya jambo hilo moja tu, Mungu anipe mtoto. Akili yangu ilikuwa ikinishawishi kwamba hata kama si mapenzi ya Mungu anifanyie kile ninachomuomba, basi atanijibu kwakua nimemng’ang’aniza. Kweli Mungu alitupatia watoto na furaha ya ndoa yetu ikawa imekamilika.

 Miaka mitatu ya mwanzo baada ya kujifungua hatukuwahi kupata changamoto, hata ya kuuguliwa kidogo na mtoto wala usumbufu wa watoto kulia au kukataa chakula. Maisha yangu ya ndoa na familia yalikuwa yenye furaha sana, amani na raha muda wote. 

Nilijiona nimependelewa kwakweli, na sikuwa na chochote cha kulalamika. Kareen na Karitta walikuwa kama maua yanayonukia ndani ya familia. Mabinti zetu hawa walizidisha furaha yetu na upendo kati yetu. Unajua kwa mwanaume kama Geof, nisingewahi kujua jinsi gani anapenda watoto mpaka Mungu alipotupatia watoto. Upendo wake kwangu ulizidi, kila mara akinishukuru kwa kumzalia mabinti wazuri. 

Pia alionekana kuwafurahia sana mabinti zake kiasi kwamba alikuwa mchangamfu na mwenye furaha muda wote. Sikuwa naona kama kuna chochote kinaweza kutokea kutuhuzunisha, kwani sasa niliona Mungu ameamua kunipa raha kila eneo.

Sikujua kuwa nina adui, shetani, adui ambaye hanipendi na daima huniwazia mabaya. Sikujua vita yangu ni kubwa kiasi gani. Nilipoona amani na utulivu, akili yangu iliamini sana juu ya ile shwari iliyoonekana kwa macho kuliko shari iliyojificha. 

Ingawa sikuacha kuomba, lakini nafsi yangu ilisahau kabisa kama tunaishi dunia yenye changamoto za hapa na pale. Sikuhisi kuwa kuna siku ndani ya sekunde furaha yangu ingegeuka kuwa huzuni, tena huzuni ya kudumu kwa muda mrefu. 

Wasiwasi niliokuwa nao kabla kuhusiana na wanaume haukuwepo tena kwani Geof alishanihakikishia kwa matendo yote kuwa ananipenda na kamwe hangebadilika. 

Wasiwasi wa ugumba pia nao ulishaisha kwani sasa hata nisingepata mtoto mwingine zaidi, tayari niliridhika. Wasiwasi wa uchumi au kazi haukuwepo kabisa, mume wangu na mimi sote tulikuwa na kazi nzuri za kututosheleza.

Nilipofika nje kule walikokuwa wakicheza watoto, nilikuta Karitta ameanguka chini na mate yanamtoka 
 
ITAENDELEA
#TrueStory

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts