Home » , » Nguvu ya Dhaifu - Sehemu ya 02 ( Simulizi ya Kweli)

Nguvu ya Dhaifu - Sehemu ya 02 ( Simulizi ya Kweli)

Written By Bigie on Wednesday, March 7, 2018 | 1:43:00 PM

Mwandishi: Grace G. Rweyemam 
Nilipofika nje kule walikokuwa wakicheza watoto, nilikuta Karitta ameanguka chini na mate yanamtoka, mwili umekakamaa.

 Mimi nilitangulia kufika halafu Geofrey akawa nyuma yangu. Ile kelele niliyopiga, sidhani kama kuna ya namna hiyo Geof aliwahi kusikia kabla. Niliita kwa nguvu sana, Yesuuuu. Kichwani niliwaza ni kifafa, lakini mtoto alionekana kama tayari amekufa. Namshukuru Mungu nina mume asiyepaniki kama mimi. 

Tulipakia mtoto kwenye gari na kwenda hospitali haraka sana. Kareen alimshika dada yake huku akilia tu tukiwa kwenye gari, akijitahidi kumuamsha. Nilihisi tumbo la kuhara limenishika, halafu likawa linakata tena kama tumbo la uzazi. Akili ilizunguka kwa mawazo. Nilijaribu kuomba ila maombi yaligoma kabisa. 

Unajua ni vyema kuwa mtu wa maombi wakati hali ikiwa shwari kabisa, kwani linapotokea janga, hujui kama utapata hizo nguvu za kusali. Geof aliendesha gari huku akikemea na kuomba kwa sauti. Nikawa tu nikiitikia amen lakini akilini hata sijielewi.

Tulifika hospitali moja, sitaitaja jina, wakampeleka chumba cha wagonjwa wa dharura yaani emergency na kuanza kumshughulikia. 

Walipima vipimo vya awali na kusema hawaoni kitu, wakawa wanamuhudumia tu kwa dripu na mashine za kupima mapigo ya moyo. Kesho yake kuna daktari alikuja na kumpima vipimo vingine pia akasema haoni tatizo, akadai inawezekana ni kifafa tu, wakati huo mwanangu hajitambui na hali iko vilevile. Sikuwa na uzoefu sana kuhusu kifafa lakini kwa uelewa wangu nilihisi ingekuwa kifafa basi angeshapata fahamu. 

Nilikasirika, tukalazimisha siku iliyofuata tumtoe mtoto, tukamuhamishia hospitali nyingine. Walipopima waliona malaria iliyoingia kwenye ubongo. Kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano malaria ni hatari sana, na hii nadhani wazazi ni muhimu kutilia mkazo zaidi. Tatizo pia kuna wakati hospitali vipimo vya malaria vinaonyesha hasi (negative) hata wakati ipo (positive). 

Kwa bahati mbaya sana wakianza kumtibu walidai ugonjwa huo umeshaathiri sehemu ya ubongo wake na hivyo kunitahadharisha kuwa huenda atakapoamka asiwe kama alivyokua zamani, yaani awe amepoteza kumbukumbu na uwezo wa akili. Hiyo ni siku ya pili tangu tumhamishie hiyo hospitali nyingine na hakuwa bado ameamka.

Nimekaa wodi ya wazazi zaidi ya masaa kumi, na ninajua vizuri uchungu wa kuzaa. Kwa mwanamke aliyezaa kwa uchungu anaweza kunielewa vizuri ninaposema tumbo la uzazi. Nikipewa taarifa kuwa mwanangu ana tatizo la ubongo na hatarudi katika hali yake ya kawaida, niliumwa tumbo sawa kabisa na lile nililoumwa wakati najifungua. 

Akili yangu ni kama ilipigwa ganzi kwa dakika halafu nikaanza kutoka machozi huku nikiwa hata sielewi kama yanatoka. Picha ilinijia ya Karitta wangu mchangamfu na mrembo kama mama yake, anayependa mambo ya mitindo na mwenye kujiamini kwa hali ya juu. Halafu nikakumbuka akiwa ndio ameanza shule aliona fahari sana kutuonyesha kuwa anajua kila kitu kuliko watoto wenzake darasani, na kuliko hata dada yake, Kareen. 

Unajua hata kama watoto ni mapacha wa mfuko mmoja, kila mmoja ni tofauti kabisa na mwenzake. Kama mama, nilielewa utofauti wa wananngu kwa ukaribu kabisa, na huo ndio ulinifanya nijiisi fahari sana kuwa nao wote wawili. Kwangu au kwetu kama wazazi, kila mmoja alikuwa wa kipekee sana. 

Hakuna ambaye alionekana bora kuliko mwenzake na hakuna aliyeonekana duni kwa mwenzake. Katika umri wao mdogo, kila mmoja nilijua vipaji vyake na nini anaweza kufanya kwa ubora zaidi.

Nilimuomba daktari aniandikie rufaa ya kwenda Afrika ya Kusini au India au Uturuki nikamtibu mwanangu, kwani nilihisi kutakuwa na ubora zaidi wa matibabu kwa nchi hizo, lakini alishauri kuwa kuna dawa ambazo walianza kumpa zingeleta matumaini na hazikuhitaji mtoto asumbuliwe kusafiri. 

Katika hali yake, kama angesafiri, ingelazimu kuchukua ndege ya ambulance ambayo ingetugharimu sana. Hakukuwa na gharama kubwa kwa binti yangu kwakweli, ingawa tulikuwa na bima lakini bima haikuwa tayari kugharimia bila daktari kuhakikisha kuwa wameshindwa na inabidi mtoto aende nje ya nchi, vinginevyo ingetubidi kulipa pesa yetu wenyewe.

Siku Karitta aliyofumbua macho na kunitazama sikuamini, ikiwa ni siku ya nane tangu aanguke. Nilimsogelea na kumuita lakini hakuonekana kunielewa, au labda hata kunisikia. 

Sasa badala ya kufurahi mtoto kafumbua macho, ni kama nilihakikisha kuwa kile alichosema daktari ni kweli, nikaanza kulia kwa uchungu. Muuguzi alikuja na kunikuta nalia, akanikataza kabisa kulia hasa mbele ya mtoto kwani nitamjengea picha mbaya kichwani.

ITAENDELEA
#TrueStory 

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts