Home » , » Nguvu ya Dhaifu - Sehemu ya 03 ( Simulizi ya Kweli)

Nguvu ya Dhaifu - Sehemu ya 03 ( Simulizi ya Kweli)

Written By Bigie on Thursday, March 8, 2018 | 10:25:00 AM

Mwandishi: Grace G. Rweyemam 

Mwanangu aliamka wiki ya tatu akiwa hawezi kuzungumza tena, upande wake mmoja wa mwili haufanyi kazi na hawezi hata kukaa tena. Sura yake ilibadilika na kuwa kama ya mtoto mwenye ugonjwa wa akili na alitoka mate muda wote. 

Vilifanyika vipimo kadhaa, mwisho ikaonekana ni vyema tukimpeleka Uturuki. Zilifanyika taratibu, tukampeleka Karitta Uturuki kwa matibabu, ikaonekana ana kovu kwenye ubongo ambalo haiwezekani kutolewa. 

Alipewa dawa kadhaa ambazo angetakiwa kutumia kwa kipindi kirefu kwenye maisha yake au labda maisha yake yote. Tulirudi Tanzania tukiwa familia iliyogubikwa na huzuni kubwa kana kwamba maisha hayana tumaini tena. 

Geofrey mume wangu ambaye siku zote ndiye alikuwa nguvu yangu sasa ndio alishuka moyo kuliko hata mimi. Nadhani tukiwa tunaenda Uturuki tumaini lake kubwa aliliweka kwa ubora wa hospitali na wataalamu wa nchi hiyo, sasa baada ya kuona huko nako imeshindikana, alipoteza tumaini kabisa.

Usiombe mwanaume apoteze nguvu za kusimama kama mwanaume na mtu wa kukutia moyo wakati wa tatizo, yaani unaweza uone ukubwa wa tatizo umeongezeka mara mbili Zaidi. Geof alinifanya nione kama siwezi kabisa kuishi na ile hali ya Karitta. Furaha ya nyumba yetu ilizima ghafla kama mshumaa, na huzuni kubwa kutufunika. 

Kimya kilikuwa kingi kuliko maongezi, tofauti kabisa na awali. Kila mmoja wetu hakuwa na maneno ya kusema, na mara zote maombi yetu yalikuwa ni kulia zaidi ya kuomba. Watu wengi walikuja nyumbani na kumfanyia maombi mtoto, na kututia moyo, lakini kuna ambao walitukatisha tamaa pia. 

Kuna mama mmoja siku moja alikuja akamuona binti yangu, tukiwa ndio tumetoka Uturuki, nikamuelezea jinsi madaktari walivyosema, akanijibu, “Mshukuru Mungu aliyekupa mapacha mama Kareen. Huyu naona maisha yake ndio hayo Mungu ameyapanga na hamna namna ya kufanya, sasa usiumie sana, angalau unaye Kareen.”

Akilini nilijiuliza hivi huyu mwanamke anaelewa uchungu wa mtoto au anaongea tu? Haikuniingia akilini kuwa mwanamke anayejua nini maana na nafasi ya mtoto kwa mzazi anaweza kusema maneno ya namna hiyo. 

Kwake kupuuza kile kilichotokea kwa mwanangu ilionekana ni jambo rahisi sana na alihisi huenda ninaweza tu nikaamua kuifunga akili yangu na kumsahau Karitta wangu. Unajua unaweza ukawa unapita sehemu, ukakutana na watu kumi wa kukutia moyo, lakini mtu mmoja tu akitokea akakuvunja moyo unaona kama hakuna tumaini kamwe tena. 

Siku hiyo baada ya kuondoka huyo mwanamke nililia haijawahi kutokea. Mume wangu alikuja na kukuta ninalia sana, akanibembeleza, nikamuelezea kuhusu yule mwanamke, lakini cha ajabu yeye hakumchukulia vibaya kama ambavyo mimi nilichukulia. Alinitaka nimuelewe tu na nijitie nguvu.

Baada ya muda ilinilazimu kuacha kazi ili nimuhudumie binti yangu vizuri. Sikumuamini binti wa kazi wala mtu yeyote, nilihisi mwanangu ananihitaji na yeye ni bora kuliko kazi. Tulijaribu tena kumpeleka mtoto Afrika ya Kusini, na baadaye India kuangalia kama huenda kunaweza kukawa na matibabu au jibu tofauti, lakini kote tulikoenda walitupa majibu yale yale na tumaini letu likazini kufifia. 

Mwaka mzima ulipita, hali ya Karitta wangu ikiwa haina nafuu yoyote. Alijisaidia hapo hapo, hakuweza kujilisha, hakuzungumza, mate yalimtoka, hakuweza kukaa na alionekana akili haiko sawa. Sikumbuki siku hata moja ndani ya huo mwaka wote ambayo sikuwa na huzuni. 

Niliona Mungu ameniacha kabisa, maombi yangu yalikuwa ni kulia tu na tofauti na nilivyo, sikuwa na maneno ya kuomba. Niliingia chumbani mara zote na kumwambia Mungu, mponye mwanangu ninaomba, naumia sana, kisha nililia tu na sikuweza kuomba zaidi.

Familia yetu, yaani ndugu zangu, ni watu ambao wameolewa na kuoa na huishi mikoa na nchi nyingine. Ni kaka yangu mmoja tu ambaye anaishi Dar es Salaam nilipo, lakini ndugu zangu wengine wote ni wa mbali. 

Baba na mama wote walishafariki, na mume wangu pia wazazi wake wote walishafariki, naye ana dada mmoja ambaye anasoma Norway. Kipindi chote nauguza watu ambao waliweza kuwa karibu na mimi ni marafiki zetu tu, lakini nadhani utaelewa kwa kuuguza zaidi ya mwaka mmoja, si rahisi ubaki na watu karibu tena. 

Ni kama watu wanaanza kuona kuwa sasa hayo ndio maisha yenu hivyo inawalazimu mzoee tu. Baada ya mwaka nilikuja kugundua kuwa hata wale marafiki wa karibu ni kama hali ya mtoto haiwahusu tena, na sasa ni mimi na Geofrey wangu tu. 

Nilimuhurumia Kareen ambaye siku zote alitumaini kuna siku dada yake atarudi katika hali ya kawaida. Hakutaka tena kwenda shule bila ndugu yake na alianza kuwa mtoto mnyonge na mpole sana. Huzuni ya kuuguliwa na pacha wake ilionekana sio tu kwetu wazazi wake, bali hata kwa watu baki waliomfahamu.

Baada ya mwaka kuisha, niliamua sasa nitaanza kuwa naenda na mtoto wangu kanisani. Awali niliona kama ningemsumbua, hivyo siku za ibada tulipokezana na baba yake, akienda ibada ya kwanza basi mimi nitaenda ibada ya pili ili mmoja kati yetu abaki na Karitta. 

Nilipoanza kwenda naye kanisani siku za mwanzoni nilihisi uchungu sana, kwani nilikumbuka siku ambazo walifika kanisani na kukimbilia kwenye darasa lao la watoto, na jinsi ambavyo walimu wao walimsifia kwa kuwa makini na haraka kujibu maswali na kuchangia mada darasani. 

Nilijitia nguvu na kudhamiria kuwa nitakuja naye tu kanisani bila kujali kuwa ilinilazimu kumpakata muda wote wa ibada. Sasa ni kama nilianza malezi ya kichanga, yaani mara kadhaa kutoka nje kumbadilisha nguo alipojisaidia.

Siku moja, ikiwa ni miaka miwili na miezi miwili imeshapita tangu mwanangu augue, na hali yake ikiwa hainamabadiliko kabisa, tukiwa kwenye ibada, alisimama dada mmoja mgeni kuhubiri. Ibada hiyo ni ya kiingereza, na huyo mgeni hakuwa mtanzania, bali mkenya anayeishi Marekani. Mchungaji wetu na mkewe waliwahi kutembelea Marekani mara kadhaa na yule dada na mumewe wakawakaribisha kwao, hivyo walikuwa marafiki. 

Hakuwa mwanamke mkubwa kwa muonekano, umri wake ulipata miaka arobaini ingawa alionekana mdogo kiasi kuliko umri wake. Yule dada akihubiri, alitoa ushuhuda wa maisha yake binafsi kwa kifupi, ukanigusa sana. Alidai alikuwa kiziwi kwa miaka 18 ya maisha yake, lakini Mungu akamfungua. 

Alielezea kuwa siku zote akiwa hasikii kabisa, mama yake alimfundisha katika lugha aliyoielewa juu ya upendo wa Mungu, na alimjua Yesu akiwa kiziwi, alibatizwa na kujazwa Roho mtakatifu akiwa kiziwi. Alianza kuumwa akiwa na umri wa miaka miwili, alifunguliwa akiwa na miaka ishirini.

Akielezea kifupi kuhusiana na namna alivyofunguliwa, “Mama yangu alinipeleka kwenye maombi na maombezi kadhaa lakini sikuwahi kufunguliwa, na ndipo alipoamua yeye mwenyewe kuwa atanisaidia mpaka Mungu aniponye. Aliamini ni mapenzi ya Mungu mimi niwe mzima tena, hivyo akaanza kunifundisha juu ya mapenzi mema ya Mungu kwangu. 

Kisha alianza kunifundisha kuhusiana na nguvu ya Mungu kuponya na jinsi ambavyo kupitia maombi ninaweza kuisababisha hiyo nguvu ifanye kazi maishani mwangu. Nakumbuka nikiwa na umri wa miaka 16, nilianza kuelewa kuwa ninao uwezo wa kusababisha nguvu ya Mungu ya uponyaji ifanye kazi kwenye maisha yangu kwa Jina la Yesu Kristo. 

Hili somo lilikuwa gumu kwangu sababu sikuwa nasikia, hivyo sikuwa najua vitu vingi. Imani yangu haikuwa imara sana, lakini baada ya miaka miwili mizima, nilianza kujengeka kiimani. Mama yangu alinitaka nijisimamie, na alinisaidia kujisimamia. 

Ndani yangu kiu ya uponyaji ilijengeka na kupitia maandiko nilielewa kuwa Mungu anaweza na anataka kuniponya, hivyo nikaanza kumuomba Mungu ninayejua ana uwezo na utayari wa kuniponya.

ITAENDELEA
#TrueStory 

Advertisement
hapa

Post your Comment

Habari Mpya

Popular Posts